Na Rajab Mkasaba
UMOJA wa Afrika (AU), umeeleza kuridhika kwake na uchaguzi wa Zanzibar uliomalizika hivi karibuni na kusema kuwa ulikuwa ni huru na salama.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mhe. Dk. Jean Ping aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Ping alimueleza Dk. Shein kuwa (AU), inajivunia jinsi zoezi la uchaguzi wa Zanzibar lilivyokwenda vizuri na hatimae wananachi kuwachagua viongozi wao wanaowataka kuwaongoza akiwemo yeye Dk. Shein.
Aidha, Dk. Ping aliendelea kutoa pongezi zake kwa niaba ya AU kwa Dk. Shein kufuatia kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Dk. Ping akiwa na ujumbe wa baadhi ya viongozi wa Tume hiyo waliofuatana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu, alieleza kuwa uchaguzi wa Zanzibar ni kigezo kikubwa kwa nchi nyengine za bara la Afrika.
Dk. Ping ambaye alikuwepo Zanzibar kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa AU ambao miongoni mwa mada zake kuu ilikuwa ni kuzungumzia amani na usalama kwa nchi za Bara la Afrika. Katika maelezo yake Dk. Ping alieleza kuwa amevutiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira ya Zanzibar ambayo ni kivutio kikubwa kwa wageni.
Balozi Mwapachu alieleza kuwa kutokana na ushindi wa Dk. Shein ana matumaini makubwa kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utaendelezwa na kwa vile Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia, Zanzibar ni kituo kizuri cha mikutano ya Kimataifa hivyo ameahidi kuwa mikutano mengine kama hiyo itaendelea kufanyika hapa Zanzibar.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein alitoa pongezi kwa ujio wa kiongozi huyo pamoja na kuichagua Zanzibar kufanya mkutano huo wa Kimataifa.Dk. Shein alisema kuwa uchaguzi uliomalizika Zanzibar ulikuwa huru na salama na kutoa shukurani kwa salamu za pongezi kutoka kwao.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta za maendeleo na changamoto iliyopo hivi sasa ni kuziimarisha zaidi.Kutokana na mafanikio hayo, Dk. Shein alieleza kuwa hatua kubwa iliyopo hivi sasa ni kushirikiana kwa pamoja ili kuziimarisha sekta hizo za maendeleo kwa ajili ya kupata mafanikio zaidi.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kufanyika kwa uchaguzi huru, salama na amani kutawezesha makubalianno ya kuwepo kwa Serikali ya Kitaifa yaende kama yalivyokusudiwa ili kuwezesha kufanya kazi kwa mashirikiano.
Akieleza juu ya vivutio vilivyopo Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina vivutio vingi ambavyo inawapelekea wageni wengi kuipenda ikiwa ni pamoja na historia yake.
No comments:
Post a Comment