Asema hainufaishi nchi, yaneemesha wajanja
Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, amesema kumekuwepo misamaha holela ya kodi kwa wawekezaji.
Waziri huyo alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na Watendaji wa Mamlaka ya Kusimamia Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), ikiwa ni mfululizo wa ziara zake za kuzitembelea Idara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.
Waziri Mzee alisema umekuwepo utaratibu wa usioridhisha juu ya misamaha ya kodi inayotolewa kwa wawekezaji wanaoingiza vitu mbali mbali, ambayo imekuwa mtaji mkubwa wa kuwanufaisha kiujanja baadhi ya watendaji.
Alisema hali hiyo inatokana na udhaifu wa sheria inayotumika kusimamia uwekezaji Zanzibar kupitwa na wakati kwa kutoa upendeleo mkubwa wa misamaha ya kodi.
Alisema kutokana na udhaifu huo wa sheria, umekuwa ukitumika mwanya wa misamaha ya kodi ambayo inanufaisha wachache, huku akisema sheria hiyo inahitaji kungaliwa upya ili kuziba mapato ya Serikali.
“Sheria iliopo inatoa mwanya mkubwa wa kumnufaisha muwekezaji kiasi ambacho wameonekana kulifanya eneo la uwekezaji kuwa kama ni pango la kujinufaisha wao binafsi badala ya Serikali”,alisema waziri huyo.
Akitaja miongoni mwa udhaifu wa sheria hiyo ni viwango vidogo vya kodi ya ardhi ambapo hutolewa za kimarekani 200,000 ambapo ni kiwango kidogo sana, huku wawekezaji wengine wakisamehewa kodi ya ushuru wa uingizaji wa magari yaliyokwisha tumika.
Alisema sheria mpya inahitajika kwani iliyopo hivi sasa haijaainisha aina ya misamaha ya kodi inayotakiwa kutolewa katika ushuru wa uingizaji wa magari nchini.
“Utaona muekezaji anaingiza gari ya Saloon iliyokwisha tumika anasamehewa ushuru, lakini hapo hapo na mwananchi Mzalendo naye akiiingiza gari anatozwa ushuru kamili hapa pana matatizo”, alisema Waziri huyo.
Akiendelea alisema eneo jengine alilitaja ni la uingizaji wa vitu kwa ajili ya kutumika mahotelini ambapo muekezaji husamehewa kila baada ya muda jambo ambalo linapaswa kufanyiwa mabadiliko kwa vile misamaha inatakiwa kutolewa mara ya kwanza mradi unapoanza.
Alisema maeneo mingine ni la misamaha ya inayohusu ujenzi wa marekebisho ya majengo kutokana na baadhi ya wawekezaji kila baada ya miaka 10 huomba kurekebisha majengo yao na kutaka kusamehewa vitu wanavyoingiza wakati awali alipewa msamaha.
Alisema ujanja mwengine ambao umekuwa ukitumiwa na wawekezaji hao kudai misamaha vitu vya ujenzi ya kujenga hoteli lakini wanapopewa hujenga vijumba 10 ambavyo havilingani na mali ya msamaha aliopewa.
Akizungumzia kodi za ardhi nazo alisema ni zenye kusikitisha kwani zimeshindwa kuangalia mazingira ya maeneo muhimu kwani viwango vya sehemu ya bahari ni sawa viwanja vya nyumba ziuzwazo mjini.
Waziri huyo aliagiza Idara hiyo ndani ya mwezi mmoja wanaanzisha mabadiliko ya sheria ya uwekezaji ili iweze kuwasilishwa katika kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi.
Mapema Mkurugenzi wa Idara hiyo, Salum Khamis Nassor, alisema kumekuwa na mgongano mkubwa wa kutofautiana kwa baadhi ya mambo kitaasisi kiasi cha kusababisha kuvutana kisheria.
Alisema hali hiyo imekuwa ikijitokeza kiasi ambacho hivi sasa baadhi ya Wawekezaji kutaka kuipandisha Mahakamani Idara hiyo huku kukiwa na mivutano katika vijiji na Wawekezji wazalendo ambao huuza maeneo bila ya kuzingatia vibali wanavyowapa awali.
Mkurugenzi huyo alisema hali ya Zanzibar kiuwekezaji bado haijawa nzuri kwani bado hawajaweza kuingia katika masoko ya kimataifa kwani hata ripoti za kimataifa zimekuwa zikionesha hivyo kunakosababishwa na baadhi ya taasisi kutokuwa na ushirikiano.
No comments:
Post a Comment