Habari za Punde

SAKATA LA KUVAMIWA ARDHI MTENDE LAMFIKIA MKUU WA WILAYA

Na Ameir Khalid

HATIMAYE wananchi wa Mtende, wameliwasilisha rasmi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kusini sakata la kuvamiwa ardhi ya kijiji hicho katika eneo la Kichangani.

Katibu wa kamati shirikishi ya shehia ya Mtende inayolinda na kusimamia rasilimali za pwani (ICM) Mussa Makame Bam, alithibitishwa suala la kuwasilishwa mezani kwa Mkuu huyo suala la ardhi yao iliyovamiwa, ili kupata maamuzi yenye maslahi kwa wananchi wa kijiji hicho.

Bam alisema madhumuni ya sakata hilo kulifikisha kwa mkuu huo, ni kutaka Serikali ya Wilaya ichukue hatua za kisheria kwa kuhakikisha ardhi hiyo inarudi mikononi mwa wananchi wa Mtende.

Katibu huyo alifahamisha kuwa hawana nia ya kukataza uwekezaji katika kijiji chao, ila hawako tayari kuruhusu uwekezaji wenye hila ya kuvamia na kujimilikisha ardhi kwa wageni.

“Tupo tayari kumkaribisha muwekezaji kuja kulima au kujenga, lakini aje kwa kufuata sheria za kijiji na sio kufuata baadhi ya watu wakafanya udanganyifu, ni lazima wafuate sheria za ardhi kwa kupata hati miliki iliyo halali ili na sisi wanakijiji tuweze kufaidika na uwekezaji huo’’alisema.

Akielezea sakata la kuvamiwa kwa eneo la Kichangani, katibu huyo alisema amejitokeza mtu mmoja ambaye ameshirikiana na baadhi ya wazawa wa Mtende kuchukua eneo hilo bila ya kufuata sheria.

Alisema mtu huyo ambaye ni mgeni kijijini hapo, alishirikina na mwenyeji huyo, kwa kulihodhi eneo hilo la ardhi lisilopungua ukubwa wa ekari 10 na kulima mazao ya chakula na biashara bila ya ruhusa ya wakuu wa kijiji hicho, pamoja na kuwa na hatimiliki ya eneo hilo.

Alisema mtu huyo aliyechukua eneo hilo alijifanya ni ni mfadhili wa kusaidia miradi ya kilimo kwa mwenyeji huyo, ambapo baadae aligeuka kwa kuwa na mipango ya kutaka kumiliki eneo hilo siku za hapo baadaye.

“Tulipoona mambo yanageuka kutoka kwenye ufadhili na sasa kuelekea katika umiliki, ndipo tulipolifikisha kwa Mkuu wa Wilaya suala hili”, alisema Bam.

Aidha katibu huyo aliwataka wananchi wa Mtende wawe wastahamilivu na kuacha kuchukua maamuzi ya jazba huku Serikali ya Wilaya ikiendelea kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

Kwa upande wao wananchi wa Mtende waliozungumza na gazeti hili wameunga mkono hatua za wakuu wa kijiji hicho kuendelea kudhibiti na kuzilinda rasilimali za kijiji hicho.

Wananchi hao walisema suala la kuilinda ardhi yao ni muhimu isijekuwa kama ilivyotokea Kigaeni Makunduchi ambapo aliwahi kutokezea mtu aliyeibuka na hila kama zinazotaka kutokea Kichangani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.