Mohammed Mhina wa Polisi, Zanzibar
KITUO cha Polisi cha Mkokotoni katika Wilaya ya Kaskazini A mjini Unguja, kimeteketea kwa moto uliotokana na hitalafu ya umeme kwenye paa la kituo hicho.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kasikazini Unguja, Mselem Masudi Mtulia, alisema tukio hilo lilitokea saa 7.30 usiku wa kuamkia jana.
Alisema askari wa zamu katika kituo hicho na wengine waliokuwa katika hali ya utayari kwa ulinzi katika eneo linalozunguuka kituo hicho, walifanya jitihada za kumuokoa mahabusu mmoja aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kupatikana na bangi.
Kamanda huyo alisema karibu mali vitu vyote vilivyokuwa katika kituo hicho zikiwemo baadhi ya bunduki na mabomu ya machozi, vimeteketea kwa moto.
Kamanda Mtulia alisema hata hivyo moto huo ulidhibitiwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji cha Mahonda katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kushirikiana na askari Polisi na wananchi wa maeneo jirani.
Hata hivyo Kamanda huyo hakutaja hasara halisi iliytokana na kuteketea kutokana kwa mali katika kituo hicho.
Usiku huo huo, Kamishna wa Polisi Zanzibar alikwenda katika eneo la tukio na kuagiza shughuli za kiusalama ziendelea kama kawaida ikiwa ni pamoja na kuwahudumia watu wanaoathiriwa na matukio ya makosa ya jinai na kuwakamata watuhumiwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Idi, akifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,Pembe Juma Khamisi, alitembelea eneo hilo na kuagiza kufanyika kwa ukaguzi wa mifumo ya umeme katika majengo ya serikali ili kuepuka matukio kama hilo.
Pia alimwagiza Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, kutafuta eneo kama hilo ili kujenga kituo kikubwa na chenye hadhi ili kuwawezesha polisi kutoa huduma zisizo na mashaka kwa wananchi.
Awali akimkaribisha makamu wa pili wa Rais, Kamishna Mussa alisema kuwa kituo hicho ni cha zamani na kwamba kilijengwa kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kikiwa kama gereza la wafungwa.
Hata hivyo alisema kuwa moto huo ungeweza kudhibitiwa mapema zaidi na pengine usingeweza kuleta madhara makubwa, lakini hali ilikuwa mbaya zaidi kutokana na kuwepo kwa milipuko ya risasi na mabomu ya machozi
No comments:
Post a Comment