Habari za Punde

KUTOKA BARAZANI: WANAFUNZI 265 WAFAIDIKA NA MIKOPO ELIMU YA JUU

JUMLA ya waombaji 976 waliwasilisha maombi yao kati yao waombaji 625 walikubaliwa kupatiwa mikopo baada ya kuingia Mkataba na Bodi ya Mfuko wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2009/2010.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad, alipokuwa akijibu suali la Ali Abdulla Ali (Mfenesini) aliyeuliza kwa mwaka 2009/2010 ni wanafunzi wangapi walijaza fomu za maombi ya mikopo na wangapi walibahatika kupata mikopo hiyo.

Naibu Waziri, alisema, kati ya hao waliokubaliwa wanawake walikuwa 215 na wanaume walikuwa 410 na walipatiwa mikopo baada ya kuingia mkataba na Bodi ya Mifuko ya Elimu ya Juu.

Aidha, alisema, hakuna fedha wanazotozwa waombaji wakati wanapowasilisha barua zao za maombi ya mikopo na gharama za shilingi 30,000 zinatozwa kwa waombaji ambao maombi yao yamekubaliwa ikiwa ni gharama za mkataba kati yake na mkataba wa elimu ya juu.

Hayo aliyasema alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Ali Abdulla Ali (Mfenesini) aliyetaka kujua wale ambao hawakubahatika kupata mikopo hiyo, hurejeshewa fedha hizo?

Aidha, alisema, kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Elimu inachukua hatua za haraka kuwatatulia tatizo la ulipaji wa ada za masomo wanafunzi wa Zanzibar walio katika vyuo mbalimbali nje na ndani.

Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa, alipotaka kujua hatua zinazochukuliwa na Wizara kuwaondolea wanafunzi tatizo la ulipiaji gharama za masomo ya juu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.