Na Fatma Kassim, Maelezo
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Juma Duni Haji amesema kupiga hatua kwenye sekta ya Afya nchini kunatokana na mchango wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).
Alisema washirika wa maendeleo mbali mbali wamekuwa wakisaidia katika kuikuza sekta hiyo muhimu kwa wananchi ambapo miongoni mwa hao ni Benki hiyo ambayo imeweza kufanikisha ujenzi wa ikiwemo nyumba za madaktari, vituo vya afya, pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi.
Waziri Duni, alisema hayo jana alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB uliofika kuonana naye.
Alisema licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa inayoikabili sekta ya Afya, kwa kiasi kikubwa imeweza kutekeleza miradi kwa wakati inayofadhiliwa na ADB na watahakikisha wanafanya vizuri katika miradi yote ambayo itakuja hapa Zanzibar.
Waziri Duni, aliiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kuisaidia Sekta ya afya zaidi katika nyanja mbali mbali ikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, mafunzo kwa madaktari, wahudumu wa afya, pamoja na uwezekano ya kuisadia ofisi ya Mkemia Mkuu kwa lengo la kutoa huduma zenye kiwango kwa wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Maendeleo ya ADB, Muduuli Mary, alisema kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa miradi mbali mbali hapa Zanzibar kwa kufanyika kwa ubora wa hali ya juu na kwa kumaliza kwa wakati pamoja na utumiaji kwa fedha kwa uwangalifu.
Alisema Benki yake itaendelea kutekeleza miradi yote kwa Zanzibar kwa lengo la uimarishaji wa huduma za afya pamoja na kuzidisha ushirikiano.
Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB inatekeleza miradi mbali mbali kwa njia ya mkopo kwa Tanzania na Zanzibar.
No comments:
Post a Comment