Na Abdi Suleiman, Pemba
WAANDISHI wa Habari Kisiwani Pemba wametakiwa kuandika habari za uchunguzi zinazohusiana na uzalilishaji wa mwanamke, ukatili wa kijinsia, utelekezaji, ubakaji wa watoto wa kike na kupiga vita vitendo vyote viovu wanavyofanyiwa wanawake katika jamii.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Kisiwani Pemba, Khatib Juma Mjaja, alieleza hayo alipokuwa akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu utetezi wa haki za wanawake, utawala bora na mkakati wa kukuza uchumi na kupiga vita umasikini Zanzibar huko katika ukumbi wa Tasaf Chake Chake Pemba.
Alisema waandishi wa habari hawana budi kukitumbuliza kwenye harakati za kuwatetea wanawake dhidi ya vitendo vyote vya uzalilishaji wa mwanamke na watoto, kama ubakaji, utelekezaji na ukatili wa kijinsia unaofanywa na watu waliokosa imani kwa wanawake na watoto.
Mjaja alisema waandishi wazitafute taasisi zinazoweza kutetea uzalilishaji wa mwanamke na mtoto kwa kutumia kalamu zao pale vitendo hivyo vya uzalilishaji vinapotokea ndani ya jamii ili hatua kali kuweza kuchukuliwa kwa wahalifu wa vitendo hivyo.
Alisema katika mkakati wa kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA), vyombo vya habari vinaanguka katika tabaka la tatu la ulinzi na utawala bora katika kuweka amani na utulivu ambapo ndipo tasnia ya habari ilipoangukia katika utetezi wa wanawake.
“Kama waandishi wa habari watatumia kalamu zao na kuamua kufichua maovu yote yaliyojificha dhidi ya vitendo vyote vya uzalilishaji wa wanawake na kupata haki zao za msingi basi tunaweza kujenga jamii iliyobora”, alisema Mjaja.
Alisema dini ya kiislamu haikubali mwanamke kutelekezwa, kunyanyaswa, na kufanyiwa vitendo vyote vibaya ambavyo ndani ya jamii yetu iliyotuzunguka na watendaji wa mambo hayo tunaishi nao bila ya kuwaonea aibu.
Naye Mwezeshaji wa mada juu ya Vyombo vya Habari na Wanawake na Umasikini kutoka Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wanawake, Vijana na Watoto Pemba, Rabia Rashid Omar, alisema mkataba wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake, “Cedar-Convention of the Elimination of all Forms of Descrimination Against Women”,ulioridhiwa mwaka 1985 unalenga kuthibitisha uaminifu wa Umoja wa Mataifa katika misingi ya binaadamu, heshima na usawa wa binaadamu wa jinsia zote.
Alisema historia ya mwanamke katika masuala ya kiuchumi inaonekana wazalishaji wakubwa katika dunia, Zanzibar wanawake wanafanya asilimia 51 ya watu wote ambao wanabeba majukumu katika jamii na taifa kwa ujumla ambao ni wakulima, wafanyabiashara ndogo ndogo kwa lengo la kujipatia kipato kwa ajili ya ustawi wa familia zao.
Aidha Rabia alifahamisha kuwa wanawake wengi nchini wasio na elimu hasa wale waishio vijijini, ambao hawana fursa ya kutosha ya kupata habari ambazo zingeweza kuwasaidia kuboresha kipato chao kutokanana kilimo au ufugaji.
Alisema kuwa ukosefu wa kudhibiti rasilimali kuu za uzalishaji, wanawake hukosa fursa hizo na huendelea kubakia masikini kwa wale wanaoishi vijijini, na hata wale wa mjini ambao fursa zipo na wanashindwa kujitokeza kwa wingi na hatimaye kubakia wanawake wengi wanaoendelea kuishi katika hali ya umasikini, na hatari ya maambukizo ya virusi vya ukimwi.
Aidha alisema kuwa utetezi wa haki za wanawake zinapaswa kushuhulikiwa na taasisi mbali mbali za kiserekali na zile zisizo za kiserekali kama vile TGNP, TAMWA, TWLA, ZAMEW,WEZA na PPC (Pemba Press Club)zote hizo zinapinga vikali vitendo vyote vya uzalilishaji wa wanawake pamoja na Cluab ya waandishi wa habari kisiwani Pemba , Pemba Press Club (PPC) kwa ufadhili wa shirika la The Foundation for Civil Society.
No comments:
Post a Comment