Habari za Punde

KITENGO CHA DAMU SALAMA KUIMARISHWA - DUNI

Na Fatma Kassim, Maelezo

WAZIRI wa Afya, Juma Duni Haji amesema Wizara yake itaendelea kuimarisha huduma za afya ikiwemo huduma za damu Salama katika hospitali mbali mbali.

Alisema huduma ya damu Salama ni muhimu katika hospitali na inahitaji kuimarishwa kuwa katika kiwango cha ubora kwa vile matumizi yake ni kupatiwa mgonjwa.

Aliyaeleza hayo ofisini kwake alipozungumza na ujumbe kutoka Norway ambao wanashugulika na huduma ya damu salama.

Alisema katika kuimarisha huduma za afya Wizara yake ina mpango wa kuimarisha Hospitali za wilaya pamoja na kuziimarisha zilizokuwepo na kuwa na vifaa vya kutosha kwa lengo la kupunguza msongamano katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja ili kuifanya iwe ya rufaa.

Aidha, alisema kuja kwa wataalamu hao kutoka Norway kutafanikisha kwa kiasi kikubwa utaalamu wa huduma za damu katika Benki ya damu pamoja na hospitalini na kuweza kupata ujuzi wa hali ya juu.

Pia aliwaomba wataalamu hao kusaidia sekta ya afya na kuweza kuondoa changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya hiyo, kuanzia kwa madaktari na wahudumu pamoja na kuwapatia mafunzo ya ndani na kujenga uzoefu katika kubadilishana na wataalamu wa nje.

Kiongozi wa ujumbe huo Tor Hervig, amesema wataisaidia Zanzibar katika huduma za afya ikiwa ni pamoja na mafunzo juu ya damu kwa wafanyakazi wa afya ili watoe huduma bora.

Alisema azma ya nchi yake ni kuisaidia Zanzibar katika huduma za Benki ya damu pamoja na kubadilishana wataalamu kwa wao kuja nchini na wale wa Zanzibar kwenda huko.

Mapema Meneja wa Mpango wa Damu salama Zanzibar Dk. Mwanakheir Ahmed, alisema mafunzo ya wataalamu hao wamesaidia kuimarika huduma za damu katika benki ya damu Zanzibar.

Alisema tayari wamekuwa na mfumo wa kubadilishana wataalamu na wafanyakazi kadhaa wameshafika Norway kwa kupata mafunzo zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.