Habari za Punde

DK SHEIN: MABOMU YA GONGO LA MBOTO NI JANGA LA TAIFA

Awapa pole wagonjwa waliolazwa hospitali


Asifu JWTZ kwa kurejesha usalama


Amfariji Mkurugenzi wa Manispaa Zanzibar

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametembelea eneo lililotokea miripuko katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Gongolamboto na kuwatembelea kuwapa pole majeruhi katika hospitali za Wilaya, Amana na Temeke mjini Dar-es-Salaam.

Awali Dk. Shein alizuru Kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Gongolamboto, ambapo alipokelewa na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Devis Mwamunyange, Mkuu wa Kikosi cha 511 KJ Kanali Aloyse Mwanjile na Maafisa wengine wa Jeshi. Akitoa maelezo kwa Rais, Mkuu wa Kambi alimueleza kuwa tukio hilo limesababisha mtafaruku mkubwa kwa wananchi na kutokea vifo, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali.

Aidha, alieleza kuwa mabweni ya askari wa kike na askari wa kiume yameharibika pamoja na baadhi ya nyumba za askari na kueleza kuwa hakuna mwanajeshi aliyefariki katika tukio hilo. Kanali Mwanjile aliwataka wananchi kuondoa hofu na kurudi katika maeneo yao huku juhudi za makusudi zikichukuliwa katika kuhakikisha usalama zaidi wa wananchi. Kanali Mwanjile, alieleza kuwa tayari wataalamu wako katika maeneo mbali mbali wakifanya kazi za kuyafyatua mabomu na kusisitiza kuwa kazi hiyo itafanyika kwa lengo la kuondoshea hofu wananchi. Kwa mujibu wa maelezo ya Kanali Mwanjile watu 21 wamefariki na zaidi 300 wamejeruhiwa.

Alieleza kuwa nyumba za wananchi wengi zimeathirika na baadhi ya mabomu yaliyochimba ardhini yamefukuliwa na kueleza hadi jana jioni mabomu 300 yaliweza kukusanywa. Baada ya maelezo hayo, Dk. Shein alionyeshwa na kutembezwa katika eneo la kambi hiyo iliyoharibika kwa mabomu pamoja na ghala zilizoungua. Katika ziara yake hiyo, Dk Shein alisifu juhudi zinazochukuliwa na JWTZ katika kuhakikisha usalama zaidi unapatikana katika kambi hiyo ikiwa ni pamoja na usalama wa wananchi na mali zao. Aidha, Dk. Shein alitembelea hospitali ya Wilaya Temeke pamoja na hospitali ya Amana iliyopo Ilala na kupata nafasi ya kuzungumza na baadi ya majeruhi hao na kuwapa pole pamoja na kuwatakia nafuu ya haraka. Dk. Shein alieleza kuwa janga hilo lililotokea ni la kitaifa kwani ni la watu wote na serikali inafanya juhudi zote za kuhakikisha wananchi waliofariki wanafanyiwa taratibu za mazishi na wale waliojeruhiwa wanapata matibabu. Alipozungumza na waandishi wa habari, Dk.Shein alieleza kuwa serikali inashughulikia athari zote zilizotokea kwa wananchi na kueleza kuwa kwa wale ambao nyumba zao zimeharibika kutokana na tukio hilo taratibu maalum zitachukuliwa. Aliwataka wananchi waendelee kutulia huku serikali kwa kushirikiana na JWTZ zikifanya juhudi kuhakikisha usalama zaidi unapatikana.

Dk. Shein aliwataka waandishi wa habari kutoa ushirikiano kwa kuwaelewesha wananchi kuwa hali sasa ni tulivu na wanaweza kurudi majumbani mwao. Mganga Mkuu wa hospitali ya Amana Dk. Meshaki Shemela alimueleza Dk. Shein kuwa mashirikiano makubwa yamepatikana katika kutoa huduma kwa majeruhi. Alisema jumla ya majeruhi 218 wamepokewa katika hospitali hiyo na wengine wameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupatiwa matibabu.

Nae Mganga Mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Temeke, Silvia Mamkwe alieleza kuwa jumla ya majeruhi 123 walipokewa katika hospitali hiyo ambapo miongoni mwao wamepewa ruhusa ya kurudi nyumbani na wapo waliofariki na wengine kupelekwa hospitali ya Muhimbili.

Baadae Dk. Shein alitembelea hospitali ya Agakhan mjii Dar-es-Salaam kwenda kumpa pole Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Rashid Ali Juma aliemwagiwa tindikali.

Wakati huo huo Mwantanga Ame anaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema si kweli kama serikali imeshindwa kufanya uchunguzi baada ya matukio ya kambi ya jeshi ya Mbagala kama inavyotangazwa na vyombo vya habari, kwani ilishaita wataalamu na kueleza kuwa maghala ya silaha ya Tanzania yako katika kiwango cha kimataifa.

Alisema matukio yaliotokea yamekuja kwa bahati mbaya na serikali itahakikisha inafanya uchunguzi wa kina ili kufahamu chanzo cha tukio hilo.

Aidha alisema serikali itagharamia taratibu za mazishi popote ndugu watakapoamua kuwazika watu waliofariki na huduma za afya kwa majeruhi wanaoendelea kupata matibabu katika hospitali mbali mbali.

Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange, alimueleza Makamu huyo kuwa watahakikisha jeshi linaimarisha usalama katika kambi zake ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Balozi Seif amelazimika kukatisha ziara yake kisiwani Pemba na kushiriki kikao cha Kamati ya Usalama wa Taifa ambacho kilifanyika chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete juzi.

Wakizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na madai ya kutakiwa kujiuzulu kwa viongozi wa Jeshi, pamoja na waziri wa Ulinzi, Makao Makuu ya Jeshi Upanga Dar es Salaam, viongozi wa jeshi hilo wameeleza kwamba suala hilo halimo katika taratibu za kijeshi.

Wamesema kuwa hatua za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa baada Tume itayofanya uchunguzi wa tukio hilo kutoa taarifa yake na kupendekeza hivyo.

Akitoa taarifa yake jana jioni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, alisema Serikali itatoa kifuta jasho kwa familia zilizopoteza ndugu, pamoja na majeruhi baada ya kutoka hospitali.

Aidha alisema waathirika wote waliopoteza nyumba zao watapatiwa makaazi ya muda, pamoja na fidia.

Pia Kikwete amesema Tanzania itaomba nchi marafiki kusaidia kufanya uchunguzi, pamoja na kushauri njia muafaka za kuhifadhi silaha katika makambi yote ya kijeshi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.