Habari za Punde

CHWAKA WALIA NA TATIZO LA MAJI

Na Ismail Mwinyi

WAKAAZI wa kijiji cha Chwaka wilaya ya Kati Unguja, wameilalamikia Mamalaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kushindwa kulitatua tatizo la maji linalokikabili kijiji hicho kwa miaka sasa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Abrahaman Muhimid Vuai, ambae ni mkaazi wa kijiji hicho alisema wamekuwa wakipata tabu kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo muhimu.

Alisema kutokana na kukosa huduma hiyo huwalazimu kununua maji ambapo dumu moja huuzwa kwa shilingi 300 kiwango ambacho ni kikubwa kutokana na kipato chao.

Hivyo Vuai aliiomba serikali kutafuta mbinu mbadala ya kulitatua tatizo hilo kwani alisema wamekuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji na kushindwa kutekeleza huduma za kujitafutia maendeleo.

“Ugomvi tulionao na watu wa Marumbi ni wa zamani ambao wao wamefikia hatua hata ya kuziba bomba la kusambazia maji kwa muda mrefu hali ambayo imetupa wakati mgumu wana kijiji wa Chwaka,”alisema.

Sheha wa shehia hiyo, Simai Msaraka Pinja, alisema tatizo hilo lipo kwa muda mrefu hivi sasa na linasababishwa na wawekezaji wa mahoteli ambao huziba bomba za kusambazia maji na kuzipeleka katika hoteli zao.

Aidha alisema tatizo la ukosefu wa maji safi na salama ndani ya shehia hiyo limeshafika kwa wahuskika ambapo nao wameshindwa kulitafutia ufumbuzi.

Hata hivyo, Sheha alisema kutokana na mamlaka ya maji kushindwa kulitatua tatizo wananchi waliamua kushirikiana kwa pamoja katika kuchimba kisima ambacho kitawasaidia kuwapatia maji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.