Habari za Punde

MAMA SHEIN AWATAKA WANAWAKE CCM KUENDELEZA UMOJA

Na Zuwena Shaaban, Pemba

MKE wa Rais wa Zanzibar Mwanamwema Shein, amewataka wanachama wa umoja wa wanawake (UWT)Mkoa wa Kusini Pemba, kuendeleza umoja na amani kwani ndiyo silaha tosha katika kukipa nguvu chama hicho.

Wito huo aliutoa katika ukumbi wa Umoja ni Nguvu Mkoani alipokuwa akiwahutubia wanawake wa UWT wa mkoa huo na kusema wanawake ndio walezi wakuu wa chama na umoja wao ndio dira kwa chama hicho.

Alisema serikali ya awamu ya saba imejidhatiti kukabiliana na changamoto mbali mbali katika kuwaletea wananchi maendeleo bora.

Mama Shein aliipongeza Serikali kwa kuwaongezea wanawake katika nafasi za uongozi ili nao wawe nguzo kwa wanawake wengine.

Aliwataka wazazi na jamii kwa ujumla kuwa karibu na watoto ili waweza kuwafundisha maadili mema na kuwapatia elimu itakayowafaa katika maisha ya baadae.

Katika risala yao wanawake wa UWT walisema mashirikiano makubwa na chama ndio yaliyosaidia kukipa ushindi chama katika uchaguzi mkuu uliopita.

Walimpongeza Dk. Shein kwa kuchaguliwa kuongoza Zanzibar na kusema wanawake wanatarajia mengi mazuri kutoka kwake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.