Habari za Punde

BALOZI SEIF ATAKA VIWANDA VYA SAMAKI ZANZIBAR

Aitaka Sychelles kuwekeza sekta hiyo

Abdulla Abdulla, Seychelles

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameeleza nia ya Tanzania kuendeleza uhusiano wa muda mrefu na Seychelles.

Balozi Seif aliyaeleza hayo katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa Seychelles, Danny Faure mjini Victoria.

Alisema uhusiano huo wa nchi mbili ulioanzishwa na viongozi waasisi wa Tanzania, marehemu Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Nyerere na Albert Rene wa Seychelles umeweka msingi mzuri wenye faida kwa nchi hizo.

Balozi Seif alisema mwaliko wake nchini Seychelles, zaidi ya kuhudhuria Tamasha la Kimataifa la Utalii pia unalenga kutafuta mbinu mpya za kuimarisha uhusiano katika masuala ya utalii, biashara na uchumi.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Seychelles, Danny Faure alisema Seychelles na Tanzania zina ajenda moja, hivyo zinapaswa kushirikiana zaidi na kuwa mfano katika kanda ya Mashariki ya Afrika.

Alieleza haja ya kushirikiana katika nyanja za uchumi na vita dhidi ya maharamia, wanaoteka nyara meli katika Bahari ya Hindi.

Balozi Seif alitembelea kiwanda cha samaki cha Oceana Fisheries cha Victoria na kuzungumza na uongozi wake juu ya uwezekano wa kuanzisha kiwanda kama hicho Zanzibar.

Balozi Seif alisema kiwanda cha samaki kinaweza kuwa mkombozi wa uchumi wa Zanzibar kwa kuwa uvuvi wa bahari kuu ni moja kati ya sekta muhimu kwa Zanzibar.

Alisema Zanzibar inazalisha kiwango kikubwa cha samaki kutokana na kuzungukwa na bahari, na viwanda kama hivyo vikijengwa vitasaidia kupunguza umaskini miongoni mwa wavuvi na wananchi wa ujumla.

Naye mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Seif Iddi alikuwa na mazungumzo na mke wa Rais mstaafu wa Seychlles, Mama Sarah Rene.

Katika mazungumzo yao mama hao walijikita katika masuala ya dawa za kulevya yanayowakabili watoto wa nchi mbili hizo mbili.

Mama Asha alisema ni kazi ngumu kuzuia dawa za kulevya mara moja kwa kuwa wanao mtandao mkubwa, fedha nyingi na mara nyingi hushirikiana na wakubwa.

Kwa upande wake mama Rene ambae anaongoza NGO ya kupambana na janga hilo kwa kuelimisha watoto, alimshauri mama Asha kuelimisha watoto wa Zanzibar kupitia NGO kama hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.