Na Salum Vuai, Maelezo
KIASI cha fedha zilizopatikana katika hafla ya kuichangia timu ya taifa ya soka Zanzibar Heroes, kimefikia shilingi 67,981,000 sambamba na dola za Kimarekani 17,900.
Meneja wa shughuli za michezo katika kampuni ya Future Century, Martha Enock, ametoa takwimu hizo baada ya kumalizika kwa hafla hiyo iliyofana sana kwenye hoteli ya Zanzibar Beach Resort juzi usiku.
Katika tafrija hiyo adhimu watu mbalimbali mashuhuri walihudhuria akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo na wageni tafauti kutoka ndani na nje ya nchi.
Michango hiyo ilitolewa kwa moyo wa kujitolea na kujali ustawi wa timu ya taifa pamoja na maendeleo ya soka nchini.
Aidha, mara kadhaa mgeni rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alihamasisha kwa kuwapigia upatu wadau kununua vitu kadhaa vilivyonadiwa ikiwemo picha yake.
Miongoni mwa waliochangia na kiasi walichotoa kikiwa kwenye mabano ni Azam FC (5,000,000), Carl Salisbury (6,000,000), Shirika la Bandari Zanzibar (dola 4,000), Benki ya Watu wa Zanzibar Ltd. (dola 4,000) zikifanya jumla ya shilingi 39,981,000 na dola 8,300.
Aidha mnada ulioendeshwa ulikusanya shilingi 28,000,000 na dola 500, ambapo Abubakar Bakhresa alinunua jezi ya Zanzibar Heroes iliyotiwa saini na Rais wa Zanzibar kwa shilingi 10,000,000, huku jezi nyengine ikinunuliwa na Shirika la Bandari kwa shilingi 2,000,000, PVR Decoder iliyotolewa na Multi-Choice Tanzania ikanunuliwa na PBZ kwa shilingi 2,000,000.
Kamera ya kisasa iliyotolewa na Afforadable Housing ikanunuliwa na kampuni hiyo kwa dola 500,
huku picha mbili za Dk. Shein alizotia saini zikinunuliwa na hoteli ya Zanzibar Beach Resort pamoja na Bandari kwa shilingi 8,000,000 kila moja.
Ahmada Yahya Wakili 'Shah' alijitolea kutoa nyumba bure kwa makaazi ya kocha wa timu ya taifa kwa thamani ya dola 9,600.
Waalikwa wa shugluli hiyo walitumbuizwa kwa ngoma ya Marimba Group pamoja na kikundi cha dansi cha Kazumuska Band huku MC Taji Liundi akiongoza hafla hiyo kwa umahiri mkubwa
No comments:
Post a Comment