JUMUIYA isiyo ya kiserikali ya kupambana na dawa za kulevya 'Drug Free Zanzibar' (DFZ), imezindua nyumba mpya katika shehiya ya Bububu kwa ajili ya kuwatibu vijana wanaotaka kuachana na mihadarati (Sober house).
Nyumba hiyo ilifunguliwa juzi katika hafla iliyohudhuriwa na wananchi mbalimbali wakiwemo masheha wa Shehiya za Bububu na Miembeni.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Suleiman Mauly, alisema kuwa nyumba hiyo inayowatibu vijana 24 kwa sasa, ni mbadala wa ile iliyokuweko Miembeni ambayo haikuwa na nafasi ya kutosha huku pia ikikosa uzio tafauti na hiyo mpya.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa nyumba hiyo, mgeni rasmi, Mwakilishi wa Viti Maalumu (wanawake) Mgeni Hassan Juma, alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya Zanzibar yameanza kupata mafanikio kwani jamii imeonesha dhamira ya kweli kuwasaidia vijana walioathirika.
Aidha alieleza kuwa kujitokeza kwa vijana wanaotaka kuacha dawa hizo kwa hiyari, ni jambo linalopaswa kuungwa mkono na jamii, pamoja na kuwasaidia ili wasirudie katika matumizi ya 'unga' au kuzalika kwa wateja wapya.
Alifahamisha kuwa tatizo la dawa za kulevya haliwezi kuodoka bila jamii kujidhatiti katika kuwasaidia wale wanaozitumia, kwa kuwa hao ni watoto, ndugu na rafiki zao na si vyema wakaachwa kuangamia bila kushughulikiwa ili waweze kubadilika.
"Pamoja na jitihada zetu, dawa za kulevya bado zipo na zinazidi kuingia nchini na kuathiri watoto na ndugu zetu, si mjini tu hata mashamba na Pemba nako kumevamiwa na janga hilo lazima tupambane sawasawa kulitokomeza", alifafanua Mgeni.
Alisisitiza haja ya kueneza elimu kwa vijana walioathirika na hata maskuli ili kuwakinga watoto wasikue katika mazingira ya matumizi ya dawa hizo ambazo ni hatari kwa afya na pia zinazorotesha juhudi ya nchi kujiletea maendeleo.
Mwakilishi huyo alipongeza jitihada za dhati zinazofanywa na kampuni ya Explore Zanzibar chini ya Mkurugenzi wake Maryam Olsen, ambayo imekuwa mstari wa mbele kuandaa harambee za kutafuta fedha kwa ajili ya kuwasaidia vijana hao.
Sambamba na hayo, Mgeni alieleza kufarijika kwake na juhudi za serikali kupitia Idara ya kupambana na dawa za kulevya na kurekebisha tabia na kutaka kasi ya mapambano iendelee huku mkazo zaidi ukiwekwa katika kuziba mianya inayotumika kupitishia dawa hizo.
Mapema katika risala yao, vijana wanaotibiwa katika nyumba hiyo walielezea changamoto kadhaa zinazowakabili ikiwa pamoja na kuwepo baadhi ya vijana wanaojiunga na nyumba hizo kwa ajili ya kufurahisha familia zao tu lakini wanashindwa kufuata miko ya kuzikimbia dawa za kulevya.
Aidha walifahamisha kuwa baadhi ya wazazi na watu wengine katika jamii, wanashindwa kutoa ushirikiano na pia wapo wanaodhani nyumba hizo ni za watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Walishauri serikali, taasisi na hata makampuni waone umuhimu wa kuzisaidia nyumba hizo kwani kuwepo kwao kunalenga kuwaandaa vijana wawe raia wema na kuendeleza taifa lao.
Tangu harakati za DFZ zilipoanza hapa Zanzibar, jumuiya hiyo imefanikiwa kufungua nyumba sita ambapo nne ziko Unguja na mbili kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment