Habari za Punde

SMZ: MATENGENEZO YAUFANYE UWANJA WA GOMBANI UVUTIE

Na Abdulla Ali, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewataka wasimamizi wanaoshughulikia matengenezo ya uwanja wa michezo wa Gombani kisiwani Pemba kuhakikisha uwanja huo unakuwa mpya na wa kuvutia zaidi.

Balozi Seif, alitoa ushauri huo alipofanya ziara ya kukagua matayarisho ya uwekaji wa nyasi bandia katika uwanja huo, akiwa katika ziara yake ya siku mbili kisiwani Pemba.

Alisema mara nyingi dhana ya ukarabati unaofanywa hutarajiwa kuwa utaufanya uwanja huo kubadilika na kuwa mzuri kama mpya, hivyo asingetarajia kuona baadhi ya sehemu zinaachwa na ubovu baada ya kuwekwa nyasi hizo.

Kwa hivyo, aliwataka kujipanga vizuri kwa lengo la kutafuta njia muafaka zitakazopelekea kukarabatiwa sehemu zilizo nje ya mkataba wa uwekaji nyasi ili Serikali itafute njia mbadala ya kukamilisha kazi hizo kwa ufanisi mzuri.

Mapema, Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ali Nassor, alimueleza Balozi Seif kuwa kazi za ukarabati huo zimechelewa kukamilika kutokana na mvua nyingi na kuharibika kwa mitambo ya kutengeneza kokoto kisiwani humo.

Hata hivyo, aliahidi iwapo mvua itapunguwa kazi iliyobaki itachukuwa wiki moja kukamilika na shughuli nzima ya ukarabati itakamilika katika mwezi ujao.

Uwanja wa michezo wa Gombani Pemba uko katika hatua za kuwekwa nyasi bandia kupitia msaada wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.