Habari za Punde

TUME YAUNDWA KUCHUNGUZA MIKATABA TATA MANISPAA

Meya aridhia, asema itamaliza ubishi

Na Mwantanga Ame

SAKATA la kudaiwa kuwapo kwa mikataba yenye utata ndani ya Baraza la Manispaa limeingia katika sura mpya baada ya baada ya Baraza la Madiwani kuamua kuunda kamati itayochunguza mikataba iliyofungwa na Manispaa ya Mji wa Zanzibar.

Hatua ya wajumbe hao imekuwa baada ya Meya wa Mji wa Zanzibar, Khatib Abdulrahman kuitisha kikao cha dharura cha Madiwani wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar, ambapo jana kulikutana na kujadiliana jana juu ya kadhia ya mikataba hiyo.

Agenda kuu katika kikao hicho ilikuwa ni kuangalia mapungufu yaliopo katika mikataba iliyofungwa na itakayofungwa na Baraza la Manispaa katika shughuli zake nia ikiwa nia ni kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa jamii pamoja na kufuata taratibu za sheria.

Agenda hiyo pia ilikuwa inaenda sambamba na kuwajengea imani wananchi juu ya uwajibikaji bora wa watendaji ndani ya baraza hilo katika kutoa huduma bila ya kukiuka sheria za nchi kwa vile wao ndio waliowachagua.

Meya wa Mji aliamua kuitangaza rasmi kamati ya watu sita ya Baraza la Madiwani, kwa ajili ya kuchunguza mikataba baada ya hapo awali kuundwa kwa kamati mbili za baraza hilo, kulifanyia kazi suala hilo lakini limejikuta likigonga mwamba kwa kukosa baadhi vielelezo muhimu.

Kamati ambazo zilizoundwa kufuatilia suala hilo ndani ya Baraza hilo ni ya Ujenzi na mazingira, na Kamati ya Mipango Miji ambazo mwaka huu zilianza kuifanya kazi ya kuangalia mikataba iliyofungwa katika eneo la biashara Saateni ambapo taarifa za baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo zilisema zinahitaji msaada wa ziada ili kulimaliza suala hilo.

Diwani wa Mji Mkongwe, Nassor Amin, alisema kati ya mikataba mitatu ambayo ilifungwa katika eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya biashara walioupata ni mmoja na iliyobaki hawakuipata baada ya kukosa taarifa zake hata pale walipowafuata wahusika wa suala hilo.

Alisema cha kusikitisha zaidi kuona kuna mkataba mwengine uliofungwa ambao mjenzi kwenye eneo hilo alilipa zaidi ya shilingi milioni 470 lakini kamati wala Baraza la Manispaa haina taaifa juu ya mkataba huo na halijawahi kuuona.

Alisema fedha ambazo Baraza la Manispaa inazifahamu kuingia kwake ni zile ambazo zilipatikana kwa njia ya mkopo kutoka kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambapo ulitoa shilingi milioni 300 ikiwa matumizi yake yamekuwa yakipirtishwa kisheria na hawafahamu ni kwanini fedha hizo zilipoigia hazikueleweka na baraza hilo.

Naibu Meya wa Mji wa Zanzibar, Khamis Mbarouk Khamis, alisema suala la kutofuata sheria za baraza hilo ni moja ya jambo lililochangia kujitokeza kwa atatizo hayo kwani waliofunga mikataba hiyo hawakuzingatia kanuni na sheria za baraza zinavyotaka.

Akifafanua kali yake hiyo alisema kwa mujibu wa kifungu cha 55 cha sheria ya Baraza la Manispaa kinachohusiana na mambo ya fedha kifungu (a) zinaelekeza Mkurugenzi atakuwa na mamlaka ya kufunga mkataba wa Manispaa kwa mali isiyozidi shilingi milioni 3,000,000 na kifungu cha (b), ikiwa mali itazidi thamani ya shilingi milioni 5,000,000, mikataba hiyo italazimika kupata ridhaa ya kibali cha Baraza la Madiwani.

Alisema kutokana na hali hiyo alisema mikataba yote iliyofungwa inaonekana wazi kuwa ilienda kinyume na taratibu za sheria za Baraza la Manispaa kwani hakuna kikao kilichoitishwa kutoa maamuzi hayo.

Diwani wa Magomeni, Hariri Abdalla Bori, akichangia hoja hiyo alisema suala la kuundwa kamati ya kuchunguza hilo ni jambo la msingi kwani wanapaswa kuona wanatekeleza wajibu wao kwa msingi wa kufuata ilani na sio kulitumia Baraza hilo kupitisha mambo kwa faida yake badala ya maslahi ya wananchi.

Alisema katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa mahesabu ya serikali ya mwaka 2008/2009 imeonesha kuwapo baadhi ya Madiwani waliochukua fedha za serikali zaidi ya shilingi milioni 2,000,000 na kushindwa kuonyesha vielelezo halisi vya matumizi ya fedha hizo huku wengine wakiwa tayari sio madiwani tena baada ya kuanguka katika uchaguzi uliopita.

Wajumbe wengine ambao walichangia hoja hiyo ni pamoja na Diwani Arafa Mohammed Said, aliyetaka kikao hicho kuahirishwa hadi kwanza wapatiwe mikataba hiyo waione huku Diwani wa Meya, Zubeir Juma, alieleza kazi za kamati hiyo haitapaswa kufanywa na kamati za kisekta na badala yake alipendekeza kuundwa kamati maalum.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya Wajumbe akiwemo Diwani wa Viti Maalum, Shara Ahmeid, kutokubaliana na wazo la kuunda kamati maalum bali kazi hiyo ifanywe na kamati za kiskta ikiwemo inayosimamia masuala ya fedha, sheria, Ujenzi na ustawi wa jamii wazo ambalo lilipingwa na kubakia la kuundwa kamati maalum.

Akifunga mjadala huo Meya wa Mji alisema hali ya kuundwa kamati ni ya msingi kutokana na hapo awali kamati za kisekta kushindwa kupata mafanikio iliyokusudia kuyapata juu ya kufuatilia suala hilo.

Alisema na ameamua kuunda kamati itayokuwa na wajumbe sita ambapo itafanya kazi kwa muda wa kipindi cha wiki mbili kwa kutayarisha ripoti na kuiwasilisha mbele ya baraza hilo.

Akitaja kazi ambazo itazifanya kamati hiyo ni kuichunguza mikataba iliyofungwa kama ilikuwa na hadhi, na namna ya mikataba hiyo kama inakasoro na kutoa mapendekezo ya namna bora ya mikataba yakutumika katika baraza la Manispaa.

Kutokana na hatua hiyo Meya huyo alimteuwa Diwani Kadhi Zubeir kuwa ndio Mwenyekiti, wa kamati ya kufanya uchunguzi huo na Nassor Amin kuwa ni Katibu na wajumbe ni Shara Ahmeid, Zubeir Hariri, Salma Ibada na Zubeir Juma.

Sakata na mikataba yenye utata lilizua gumzo na mabishano miongoni wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kikao kilichopita

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.