Habari za Punde

ZFA YAITUPIA MPIRA CECAFA

Yadai Zanzibar haikushindwa kuandaa ‘Kagame Cup’

Na Donisya Thomas

CHAMA cha soka Zanzibar (ZFA), kimewajia juu wale wanaodai kuwa kimeshindwa kuandaa mashindano ya Kombe la Kagame, na kusema hawajui wanachokisema bali wana ajenda binafsi ya kukipaka matope chama hicho.

Makamu wa Rais wa chama hicho Haji Ameir, amesema watu wamekuwa wakipiga kelele kwamba Zanzibar chini ya ZFA imeshindwa kuandaa mashindano hayo, lakini akasema wanaropoka bila kufahamu undani wa kadhia hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Makamu huyo alisema si kweli kwamba ZFA imeshindwa kuyaandaa mashindano hayo, kwa vile si jukumu la nchi mwenyeji kuzisafirisha timu kutoka na kurudi katika nchi zao, bali hiyo ni kazi ya CECAFA.

Kiutaratibu, alieleza kuwa nchi inapoandaa mashindano, wajibu wake ni kuzigharamia timu kwa huduma za ndani zikiwemo malazi, chakula, usafiri wa ndani, posho za makamisaa na waamuzi, na sio kuzipandisha ndege.

"Hakuna hata nchi moja inayosafirisha timu katika mashindano hayo bali CECAFA yenyewe ndiyo inayowajibika kubeba jukumu hilo sasa sisi tunalaumiwa kwa nini wakati wenyewe wametuambia hawajapata mfadhili", alihoji.

Alisema baada ya Zanzibar kuombwa kuandaa mashindano hayo, ZFA ilizungumza na serikali na kukubaliana kuwa yafanyike hapa, lakini baadae CECAFA yenyewe ikasema haijapata mfadhili na kuongeza kuwa hiyo ndiyo sababu ya kufuta uenyeji wa Zanzibar.

Alibainisha kuwa, wakati CECAFA ikihangaika kusaka mfadhili, ndipo ilipojitokeza kampuni ya El-Merrekh ya Sudan na kujitolea kudhamini michuano hiyo kwa masharti ichezwe nchini Sudan na sio katika ardhi ya nchi nyengine.

Mashindano ya Kombe la Kagame hudhaminiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame kwa zawadi za washindi watatu wa kwanza kila mwaka, huku CECAFA kwa kushirikiana na nchi inayoandaa zikilazimika kugharamia huduma za timu wakati wa mashindano.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.