Habari za Punde

KILIMO CHA MPUNGA KUFANYIWA MAGEUZI

Na Nafisa Madai, Maelezo

WAZIRI wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yusuf Himid, amesema mipango ya serikali ni kuhakikisha hadi mwaka 2015 hekta 6,000 ziwe zinalimwa na kuzalisha mpunga ili kupunguza uagizaji wa mchele kutoka nchi za nje.

Mansoor alieleza hayo jana wizarani kwake Darajani mjini hapa, alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Yudhistirano Sungad.

Waziri huyo alisema hali ya uzalishaji mpunga Zanzibar hivi sasa haiwiani na matumizi ya mchele ambapo wakulima nchini kwa mwaka huzalisha tani 16, kiasi ambacho hakikidhi hata robo ya mahitaji ya wananchi wa Zanzibar.

Akitaja sababu zinazokwaza wakulima kutolima kwa wingi mpunga visiwani hapa ni ukosefu wa vitendeakazi, mbinu duni na ukosefu wa pembejeo za mbolea.

Aidha waziri huyo aliishukuru serikali ya Indonesia kwa uamuzi wake kuisaidia Zanzibar katika sekta ya kilimo husani kilimo cha mpunga ambapo imekuwa kilio cha wakulima wa zao hilo.

Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, alisema serikali yake imeleta wataalamu wawili nchini ili kusaidia taaluma kwa wakulima na kuweza kuzalisha mpunga kwa wingi na wenye viwango.
Aidha alisema wataalamu hao wataweza kutoa elimu ya matumizi ya elimu ya mbolea isiyo na kemikali ili kuilinda afya ya mlaji pamoja na uharibifu wa ardhi.

Balozi Yudhistirano alisema Indonesia na Zanzibar zimekuwa na urafiki wa muda mrefu, hivyo ni muhimu kutumia utaalamu iliyonao kusaidia kuinua kilimo hapa visiwani.

Mazungumo baina ya waziri Mansoor na Balozi Yudhistirano yamekuja kufuatia mazungumzo ya awali yaliyofanyika miezi miwili iliyopita, na leo hii Balozi anatarajiwa kutembelea mabonde yanayotumika kwa kilimo cha mpunga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.