Na Mwantanga Ame
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameipongeza serikali ya Zanzibar kwa kubadili historia ya sekta ya kilimo kutokana na kuamua kupunguza bei za pembejeo pamoja na kuanzisha mpango wa kuwapa ruzuku wakulima.
Wajumbe hao waliyaeleza hayo wakati wakichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo na Maliasili mwaka wa fedha 2011/2012 iliyowasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mansoor Yussuf Himid, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Wajumbe hao walieleza kuwa Zanzibar imeanzisha historia mpya kwa serikali kuamua kutekeleza kwa vitendo ahadi yake ya mapinduzi ya kilimo kwa kukubali kubeba baadhi ya gharama za kilimo.
Mwakilishi wa Koani Mussa Ali Hassan, akitoa mchango wake alisema kwa mara ya kwanza Zanzibar imejenga historia ya kuwapa nafuu wakulima kwa kuweka ruzuku kwa wakulima mpango ambao haujawahi kutokea katika Taifa hili.
Alisema anaamini hatua hii ya serikali itaweza kuwasaidia wakulima wengi hapa nchini na anaamini kuwa wakulima wote wataunga mkono uamuzi huo wa serikali.
Hata hivyo Mwakilishi huyo alisema ipo haja serikali ikaliangalia suala la kuongeza visima vya maji katika mashamba inayoyamiliki kutokana na hivi sasa wakulima wengi kushindwa kufanya kazi zao kutokana na kukosa huduma ya maji.
Mwakilishi wa Chonga, Abdalla Juma, alisema Zanzibar inaelekea katika kufanya makubwa katika kujikimu na chakula na uamuzi wa Rais wa kuweka ruzuku kwa wakulima amefanya uamuzi wa kijasiri kwani bajeti ya kilimo inatoa matumaini makubwa kwa wakulima.
“Nilisema leo nisikosoe, lakini nilisema nisimame kumsifu Mheshimiwa kwani katika hotuba hii kuna mambo muhimu ya kuendeleza kilimo kwa kuzingatia matrekta, bei za pembejeo kushuka sana, taaluma za wakulima sasa huwezi kusema wewe useme nini ila kumpongeza” alisema Mwakilishi huyo.
Hata hivyo alieleza ipo haja ya kuangaliwa matumizi ya ardhi yaliopo kutokana na kuanza kuongezeka kwa idadi ya watu ambapo inahitajika kufanywa utafiti ili kujua eneo gani linalofaa kwa kilimo kwani kuna hatari ya wananchi wakaimaliza ardhi kwa ajili ya makaazi.
Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisema bajeti ya kilimo imeweza kuonesha malengo makubwa ya serikali katika kufikia mapinduzi ya kilimo kwani uamuzi uliouchukua unahitaji kuungwa mkono.
Rais wa Zanzibar kutumia kauli mbiu hiyo alitambua matatizo ambayo hivi sasa tayari yanatokea katika dunia juu ya hali ya chakula na mpango wa kuweka ruzuku kwa wakulima utaweza kuwafanya wazanzibari kuwa katika hali nzuri ya chakula.
Alisema baadhi ya mataifa hivi sasa yameweza kufanikiwa katika kuinua sekta ya kilimo na kujitosheleza na chakula kutokana na kutumia mpango wa kuwapa wakulima wao ruzuku.
Hata hivyo Jussa aliiomba Wizara hiyo kuweka bayana juu ya mchango wa zaidi ya shilingi milioni 300, iliyopewa Tanzania katika mfuko wa wafadhili kupitia sekta ya kilimo kwa ajili ya mradi wa kukuza kilimo kama Zanzibar ilipewa fedha hizo kwa vile ulikuja kwa jina la Tanzania.
Mwakilishi wa Kitope, Makame Mshimba, alisema hatua ya serikali imeonesha dhamira ya kweli kutaka kuwepo mabadiliko ya sekta ya kilimo, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, anastahiki kupewa pongezi kwani atawasaidia wakulima wengi.
Alisema hata hivyo ipo haja serikali pia ikafikiria kuwapatia mikopo ya matrekta wakulima ikiwa ni hatua itayoweza kusaidia upungufu wa zana hizo na kuwawezesha wakulima kuwahi msimu wao.
Aidha Mwakilishi huyo pia aliiomba Wizara hiyo kulifanyia kazi vyema suala la kiwanda cha sukari cha Mahonda, kutokana na muwekezaji aliyepewa eneo hilo kuonekana ameshindwa kuzalisha sukari na badala yake amehodhi mashamba na wakulima kushindwa kufanya shughuli zao.
Nae Mwakilishi wa Wete, Asaa Othman Hamad alisema hatua ya serikali kubeba mzigo wa asilimia 70 katika gharama za pembejeo za kilimo ni jambo la kupongezwa na wakulima wanahitaji kuona wanaliunga mkono kwa kushiriki zaidi shughuli za kilimo.
Hata hivyo Mwakilishi huyo aliiomba serikali kuhakikisha inafanikisha mpango wake wa kuwa na ghala ya hifadhi ya chakula kutokana na kuwa ni moja ya jambo la msingi kwani na baadhi ya nchi duniani zimekuwa na uhifadhi wa chakula hadi cha kuwapatia wanyama wao.
Nae Mwakilishi wa Wanawake, Raya Hamad, alisema hatua ya Rais kuanza kufanya mageuzi ya kilimo ni jambo la kupongezwa kwani itawasaidia wanawake kuwapunguzia matatizo katika sekta hiyo ya Kilimo.
Mwakilishi wa Ziwani, Rashid Seif, akitoa mchango wake alisema serikali inahitaji kupewa pongezi kutokana na kuanza kazi kwa uhakika na ari kubwa kwa kuwapa unafuu wananchi kwenye kupata pembejeo kwani ni jambo la aina yake Zanzibar imelifanya.
Hata hivyo Mwakilishi huyo aliomba serikali kufikiria kuyaangalia maeneo ya mazao mengine likiwemo la nazi na viazi kutokana na hivi sasa kuwepo kwa mazao ya vyakula vya matunda kutoka nje ya Zanzibar na kuweka utaratibu mzuri wa kupata matrekta ili wakulima wayapate kwa wakati.
Mwakilishi wa Mtambile, Mohammed Khalid Hamad, aliipongeza serikali kuona imefanya mabadiliko ya pembejeo kwa wakulima kwani mabadiliko hayo yataweza kukuza kilimo hapa nchini.
Mwakilishi wa Jimbo la Mkwajuni, Mbarouk Musa Wadi Mtando, akitoa mchango wake aliipongeza Wizara hiyo kwa kufanikiwa kuandaa mpango bora wa kukuza kilimo kwa kuwapatia ruzuku wakulima wa Zanzibar.
Hata hivyo Mwakilishi huyo aliiomba Wizara hiyo kumpatia maelezo ya msingi juu ya maghala ya kuhifadhia chakula ambapo hivi sasa tayari kuna taarifa za kuwa yameuzwa.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub akitoa mchango wake alisema bajeti ya Wizara hiyo imeweza kuzingatia mambo ya msingi ya kukuza kilimo na ipo haja kwa wakulima kuipokea kwa pamoja.
Hata hivyo Mwakilishi huyo aliomba Wizara hiyo kuliangalia tatizo la nzi wa embe kutokana na hivi sasa wakulima wamevunjika moyo kuendeleza kilimo hicho.
Nae Mwakilishi wa Wawi, Saleh Hamad, akitoa maoni yake alisema serikali kwa kiasi kikubwa imeonesha nia ya kukuza kilimo lakini isiishie hapo na ingelikuwa busara kuwafikiria na wakulima hali zao za maisha kutokana na wengi wao bado ni masikini na wanashindwa na hata mlo wao.
Mapema Wajumbe wa Kamati Fedha, Biashara na Kilimo, wakiwasilisha maoni yaliyosomwa na Mwakilishi wa Kikwajuni Mahmoud Mohammed Musa, walieleza kuwa wanaipongeza serikali kwa kutoa punguzo kubwa la mbolea na huduma za matrekta kwani serikali imeweza kuwajali wakulima kutokana na vipato vyao kuwa ni vidogo na kupendekeza usambazaji wa mbegu kwa kuzingatia wakati muafaka.
Wajumbe wa Baraza hilo waliendelea kuijadili bajeti hiyo jana na baadae waziri wa wizara hiyo Mansoor Yussuf Himid kufanya majumuisho ambapo bajeti itayofuata ni ya Waziri wa ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana Wanawake na watoto itayowasilishwa na waziri wa Wizara hiyo Zainab Omar Mohammed.
No comments:
Post a Comment