Na Ismail Mwinyi
KATIBU Mtendaji Jumuiya ya kuhifadhi Mazingira Ras Fumba (FUPECO), Abdulrazak Shaaban Juma, amesema lengo la kuanzishwa Jumuiya hiyo ni kuhifadhi mazingira ya baharini na nchi kavu ili kuleta maendeleo endelevu na ustawi wa wanajamii wa Fumba.
Alitoa maelezo hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kampeni ya usafi katika maeneo ya fukwe ya bahari ya Kororo iliyopo Fumba, Wilaya ya Magharibi, Unguja.
Juma alisema kuwa jumuiya imeona kufanya usafi katika maeneo hayo kutokana na mazingira ya fukwe hiyo kuwa katika hali mbaya inayoweza kuleta athari kwa viumbe wa baharini na nchi kavu.
Hivyo, Katibu Mtendaji huyo ameeleza kuwa jumuiya hiyo imeanza kutekeleza majukumu yake ili kurejesha mandhari ya asili katika fukwe hiyo ili kuweze kupatikana kwa maendeleo ya Zanzibar.
“Tumeanza kutekeleza majukumu yetu ya kusafisha maeneo ya fukwe za baharini ambapo tutaendelea na kazi yetu hii ya kuweka usafi katika fukwe za fumba,”alieza Katibu huyo.
Aliongeza kuwa mazingira ya fukwe ya baharini hivi sasa imekuwa ikipoteza uhalisia wake kutokana na kuwepo katika hali ya uchafu uliokithiri katika mwambao huo wa bahari.
Aidha Juma alisema mazingira ya bahari hiyo yameathiriwa vibaya na utupaji taka, mifuko ya plastiki, uchimbaji mchanga na ukataji miti ovyo kwa ajili ya kutengeneza makaa.
Kuhusu changamoto kwa jumuiya hiyo, alisema ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi kama mapanga, viatu maalum, mabaro glavu kuzuia uchafu na vifaa vyengine vidogo vidogo.
Hivyo, amewataka wafadhili mbali mbali kujitokeza katika kuiunga mkono jumuiya hiyo ambayo bado ni changa ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Jumuiya ya kuhifadhi mazingira ras Fumba (FUPECO) imeanzishwa mwaka huu ikiwa na wanachama 34 wanawake 18 na wanaume 16.
No comments:
Post a Comment