Habari za Punde

KUCHELEWA HAKIMU KWAKWAMISHA KESI DHIDI YA ZFA

Na Khamis Amani

KESI inayowakabili viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imeendelea kupigwa kalenda baada ya hakimu dhamana wa mahakama ya Mkoa Vuga kuchelewa kufika mahakamani jana.


Hatua hiyo ilifikiwa baada ya makubaliano ya pande zote mbili mdai na mdaiwa, baada ya kuonekana hakimu muhusika amechelewa kufika kazini.

Hadi mwandishi wa habari hizi anaondoka mahakamani hapo saa 4:15 za asubuhi, hakimu huyo Hamisa Suleiman Hemed alikuwa hajawasili, hali iliyosababisha pia baadhi ya kesi zinazosimamiwa na mawakili mbalimbali kupangiwa tarehe nyengine na karani wa mahakama hiyo.

Hata hivyo, ni Katibu Mkuu wa ZFA pekee Mzee Zam Ali, ndiyo pekee aliyefika mahakamani hapo kwa upande wa wadaiwa, ambapo wakili wa wadai Abdallah Juma alikuwepo.

Katika kikao kilichopita, Rais wa ZFA Ali Ferej Tamim, aliiomba mahakama kuwapa muda zaidi ili wakamilishe taratibu za kuweka wakili wa kuwatetea katika kadhia  hiyo, ingawa pamoja na kukubaliwa ombi hilo, mahakama iliwataka kujibu madai yanayowakabili ndani ya kipindi hicho kilichobaki, ili kikao kitakachofuata (jana) shauri hilo liweze kusikilizwa.

Wadai katika kesi hiyo ni Amani Ibrahim Makungu, Suleiman Mahmoud Jabir pamoja na Hafidh Kassim, wanaotaka ZFA iwalipe  shilingi milioni 21, zikiwa gharama walizotumia katika kushiriki uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika Disemba 31, 2010 ambao matokeo yake yalibatilishwa baadae.

Kesi hiyo ya madai namba 13/2010 ilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili 12 mwaka huu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.