Yadaiwa waliopewa dhamana kuongoza si wanamichezo
Na Abdi Suleiman, Pemba
WADAU wa mchezo wa mpira wa kikapu kisiwani Pemba, wameonesha hofu kubwa kwamba huenda mchezo huo ukafutika katika ramani kwa kile walichodai kuwa umetelekezwa.
Mmoja wa wadau wa mchezo huo kisiwani humo Hussein Matora, amesema kwa muda mrefu sasa, mchezo huo umekosa usimamizi na kusababisha kutoweka kabisa.
Matora alisema licha ya mchezo huo kujizolea mashabiki wengi, lakini kukosekana kwa kalenda ya ligi ya kanda, wala ligi kuu ya Zanzibar, wachezaji wengi wameamua kujiweka kando na kutoendelea kuucheza.
Alisema siku hizi mpira wa kikapu umekuwa hauchezwi tena hata maskulini, kwa kuwa vijana wengi wanauona kama ni mchezo wa kujifurahisha tu na sio endelevu kama ulivyo mpira wa miguu.
Matora alifahamisha kuwa, hali hiyo inatokana na mamlaka zinazosimamia michezo nchini kutokuona umuhimu wa kuuendeleza na hivyo kuuacha ukisambaratika bila kuchukua hatua zozote za maana kuunusuru.
“Pemba sasa hakuna mashindano ya mpira wa kikapu, hata ligi ya sisimizi hakuna na wa wachezaji wamesambaratika, hii ni aibu kubwa kwa nchi na zaidi kisiwa cha Pemba ”, alifahamisha Matora.
Alieleza kuwa hali hiyo inapingana na kauli za kila mara kwamba michezo ni ajira, huku kukiwa hakuna misingi madhubuti inayowaandalia vijana mazingira ya kuajiriwa kupitia sekta hiyo, huku mafundi wa televisheni na umeme wakitafutwa kuongoza mchezo huo badala ya wanamichezo husika.
Aliwaomba viongozi wa juu wa serikali kuingilia kati suala la michezo Zanzibar, hasa mpira wa kikapu ambao pamoja na mingine iko mahatuti ikisubiri kukafiniwa na kuzikwa.
Aidha alishauri dhamana ya kuongoza michezo waachiwe waliomo katika sekta hiyo badala ya wababaishaji ambao wanachangia sana kurudisha nyuma maendeleo ya michezo Zanzibar, pamoja na kuitaka kutafuta wafadhali watakaosaidia kuufufua mchezo huo kisiwani Pemba.
Mara ya mwisho ligi ya mpira wa kikapu kufanyika kisiwani Pemba, ilikuwa msimu wa mwaka 2009/2010 ikijumuisha timu 11, zikiwemo tisa za wanaume na mbili za wanawake, lakini sasa hazijulikani zilikopotelea kutokana na kukosekana uongozi madhubuti.
No comments:
Post a Comment