Mwanasheria mkuu ataka busara itumike
Na Ramadhan Makame
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi jana walichachamaa na kuiweka katika hali ngumu bajeti ya wizara ya Makaazi, Maji, Nishati na Ardhi, ambapo wajumbe hao walihitaji ufafanuzi wa ziada ili kupitisha vifungu vya matumizi ya bajeti hiyo.
Waziri wa wizara hiyo Ali Juma Shamuhuna pamoja na kutoa ufafanuzi wa ziada uliohitajika na wajumbe hao, pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud na waziri wa Katiba na Sheria Abukakar Khamis Bakary, walilazimika kusimama mara kwa mara kujibu hoja za wajumbe hao zinazohusu sheria hasa kwenye kipengele cha mafuta na gesi.
Kabla ya kupitishwa kwa bajeti hiyo Shamuhuna, alisema kuwa msimamo wa kuling’oa suala mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano lipo pale pale na hakuna kilichobadilika.
Alisema suala la nishati hiyo kutolewa katika orodha hiyo, linamgusa kila mwananchi wa Zanzibar kutokana na umuhimu wake kiuchumi, mipango inafanyika kuhakikisha linaondolewa katika orodha ya mambo ya muungano.
Alisema moja kati ya mgogoro uliomo katika katiba ya Tanzania ni suala la mafuta, akibainisha kuwa lazima ushirikiano upatikane na kuepuka baadhi ya wengine kuonekana wasaliti.
“Napenda kuahidi, katu sitorudi nyuma katika suala la mafuta kama lilivyoamuliwa katika baraza hili, nakupongezeni sana kwa kuguswa na suala hili, meseji zenu zimefika kunakohusika na wamezisikia”.
Alisema jukumu alilonalo kwanza ni kuliondoa suala hilo katika orodha ya mambo ya muungano ambapo kwa mujibu wa katiba iliyopo hivi sasa imekuwa kipingamizi kikubwa cha uchimbaji mafuta.
Alisema Muungano umekuwa si ndoa bali ni ndoano iliyofika kooni, huku kila anachosema Mzanzibari juu ya matatizo ya muungano akitizamwa kwa jicho baya.
Waziri huyo alipendekeza mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano yatumiwe kikamilifu na yawe ajenda namba moja katika kuhakikisha wananchi wanatoa mawazo ya kuling’oa suala hilo.
Alisema kwa sasa hakuna muwekezaji anayeweza kuleta kampuni zake kuchimba mafuta Zanzibar na kuwekeza katika mafuta kutokana na kuwepo migogoro ya katiba na sheria.
Waziri huyo alisema katika awamu ya Dk. Salmin shirika la TPDC liliileta kampuni kutoka Canada kuja kufanya utafiti wa mafuta, lakini rais huyo alikataa kwani nchi hiyo iliigomea kuipa misaada Zanzibar.
Alisema yale yalio katika mamlaka yake kuhusu suala la mafuta yamekuwa yakifanyiwa kazi ambapo alieleza taarifa mbali mbali za kiutafiti zinazoendelea katika kuyatafuta katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Othman Masoud alisema suala la mafuta linahitaji umakini na kuwepo utaratibu maalum ili kuepuka machafuko kama yale yanayoshuhudiwa kutokea katika nchi nyingine.
Alisema Zanzibar inahitaji kuunda sheria ya mafuta, kwani hivi sasa haipo, ambapo sheria ya mwaka 1951, imekufa baada ya mafuta kuingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano.
“Ni muhimu jambo hili kulitatua kikatiba liwe wazi na tuweze kukaribisha wawekezaji kwenye sekta ya mafuta, hakuna njia ya mkato tusubiri marekebisho ya katiba ya Jamhuri yaje”.
Kwa upande wake waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, alisema serikali lazima ikae itafute mbinu ya kulitoa katika orodha ya Muungano kwanza halafu ndio hatua nyengine zifuate.
“Suala la mafuta limeshaamuliwa na Baraza la Wawakilishi, serikali inalishughulikia kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar, tunalishghulikia kwa nguvu zetu zote”, alisema waziri huyo.
Naye waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yussuf Himid alisema dhamira ya serikali na wananchi wa Zanzibar ni kuliondosha suala hilo katika mambo ya muungano.
“Msimamo wangu mimi ni sawa na watu wote humu ndani, sikubali leo, sikubali kesho sikubali Abadan!, ni dhambi kulikubali suala hili kuendelea kuwa katika mambo ya muungano”.
“Ajenda yetu ni kuyatoa mafuta na gesi asilia katika mambo ya muungano, narejea tena kuyatoa, hiyo ndio ajenda na msimamo wetu”,alisema Mansoor.
Alifahamisha kuwa ni wakati wa kuwaandaa wazanzibari ili wajadili upya mambo ya muungano na kueleza bayana ni mambo yepi wanayataka na yepi yatolewe, na hata ikibidi pia kuangalia mfumo wa muungano wenyewe ikiwemo kujadili serikali ngapi.
Kwa upande wake Naibu waziri wa wizara hiyo Haji Mwadini Makame alizungumzia mikakati ya wizara hiyo katika kukabiliana na changamoto za uvamizi wa ardhi.
Matatizo mengine yaliyotolewa ufafanuzi na Naibu huyo ni pamoja na umeme na maji.
Baada ya majumuisho yaliyofanywa na waziri Shamuhuna ambaye alikuwa akiwabembeleza wajumbe wa Baraza kumrejeshea shilingi, wajumbe wa Baraza hilo waliipitisha bajeti hiyo
Nyie ndio kwanza mnataka kuyangoa kwenye huo Muungano wakati wenzenu tayari wanaanza kuyatafuta.Majuzi Pinda alikwenda mwenyewe Korea kuzindua Meli ya utafiti.
ReplyDeleteNa inasemekana ule mkondo wa Mafia ndio huo huo unaotoka kule Pemba hivyo wao wakiwahi sisi tumeula na chua. Watadai ni yao
Hongera sana wabunge na wawakilishi wetu katika baraza msimamo ni huo huo tuko pamoja na nyinyi na inshalah tutafanikiwa mungu akipenda...lakini mumepata taarifa kuwa Pinda ameshakwenda south korea kwenda kukagua hilo ji Meli linalokuja mwezi ujao kwa ajili ya kutafuta mafuta katika mwambao wa pwani wote??
ReplyDelete