Habari za Punde

WANAFUNZI WAONYWA KUEPUKA HADAA ZA WENYE MAGARI

Na Mwanajuma Abdi

WANAFUNZI katika ngazi mbali wameonywa kuwapuuza watu wenye fedha wanaojaribu kuwahadaa na baadae kuwaambukiza magonjwa ya zinaa ikiwemo ukimwi na homa ya ini.

Ofisa kutoka Idara ya kupambana na dawa za Kulevya na kurekebisha Tabia, katika Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Fatma Mussa alisema hayo jana, wakati akitoa mada ya Uhusiano wa dawa za kulevya na UKIMWI.

Semina hiyo ya siku moja iliyofanyika katika Skuli ya Sekondari ya Ben Bella, iliyoandaliwa na Jumuiya ya ZAYEDESA, chini ya Ufadhili wa Aga Khan kupitia Hoteli ya Serena Inn katika mradi wa Mji Mkongwe.

Semina hiyo ilizishirikisha skuli 11 za sekondari na msingi zilizokuwepo katika Mji Mkongwe, ambazo zimewajumuisha wanafunzi 60 na walimu 10, ambapo mafunzo hayo maalum katika upigaji vita matumizi ya dawa za kulevya na kupambana na UKIMWI katika Mji huo wenye urithi wa kimataifa.

Alisema baadhi ya wanafunzi hususani wa kike wanarubuniwa na waendesha magari, zikiwemo daladala na TAXI, hali ambayo inachangia kujiingiza katika matendo maovu, sambamba na kupata maambukizi ya maradhi ya UKIMWI.

Akitoa ushuhuda wake kwa wanafunzi hao kwamba aliwahi kupanda daladala lakini mlango wa mbele ulifungwa na baada ya kuchungulia ndani alimkuta mwanafunzi amekaa na dereva pekee yake, hali ambayo ni hatari kwa vijana kujiingiza katika masuala hayo wakati bado wakiwa na umri mdogo.

Aidha alieleza wimbi la watumiaji wa dawa za kulevya linaongezeka kila uchao, ambapo katika mitaa mingi hivi sasa ni hatari kupita nyakati za jioni ukiwa unazungumza na simu ikiwemo Muembemakumbi, ambapo wazee wanawaogopa watoto wao hata wakifanya makosa wanawaona hawawambii kitu.

Alifahamisha kuwa, madawa ya kulevya yanauhusiano mkubwa kwa maradhi ya UKIMWI, hususani wanaojidunga sindano, ambapo wengi wao hawana muamko wa kutumia bomba moja mtu mmoja, hivyo hutumia kwa kupokezana.

Afisa huyo, alisema mbali ya kujidunga sindano, pia baaadhi ya vijana waliojiingiza katika matumizi hayo wanapokosa hulazimika kufanya ngono zisizo salama ili waweze kupata dawa hizo kwa vile anajiona katika mwili wake amepungukiwa.

Nae Mwanafunzi wa skuli ya Hamamni aliiomba Jumuiya ya ZAYEDESA kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupita maskuli kwa ajili ya kuhimiza uundwaji wa kamati maskuli kwa lengo la kupiga vita matumizi ya dawa za kalevya na UKIMWI, kwani vijana wengi wanapatikana huko, ambao wanakabiliwa na vishawishi vingi mitaani.

Nao walimu walitoa wito kwa wanafunzi hao kujifunza kwa mashuhuda waliotoa mada ambao walikuwa wakitumia dawa za kulevya kwa muda mrefu tokea skuli, hali ambayo imewasababishia kupoteza muelekeo wa masomo na hatimae kukimbia na kubakia mitaani.

Walisema mashuhuda hao walieleza kwa hamasa na uchungu mkubwa, hivyo wanafunzi wana kila sababu ya kijifunza kutoka kwao na kuachana matumizi ya dawa hizo pamoja na kujikinga na maradhi yasiyokuwa na tiba hadi sasa ya UKIMWI.

Walifahamisha kuwa dawa za kulevya zinaingizwa kupitia Viwanja vya Ndege, Bandari kuu na zisizo rasmi na kushauri serikali iongeze jitihada katika kuzuia matumizi na uingzaji dawa hizo nchini.

Semina hiyo, imefungwa na Katibu Mkuu Jumuiya ya ZAYEDESA, Lucy Majaliwa, aliewahimiza wanafunzi kusambaza taalum awalioipata kwa wenzao

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.