CHAMA cha mchezo wa judo Zanzibar (ZJA), kimewahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kujiunga na mchezo huo.
Katibu Mkuu wa chama hicho ambae pia ni kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Tsyoshi Shimaoka, amesema Wazanzibari wamekuwa woga sana kujiunga na mchezo huo ikilinganishwa na nchi nyengine.
Alisema wakati umefika kwa wanawake kusonga mbele kimichezo, hasa kutokana na mabadiliko makubwa duniani ambapo jinsia hiyo iko mstari wa mbele katika mambo mbalimbali.
“Wakati umefika sasa kwa wanawake wa Kizanzibari kujiunga na michezo tafauti, kwani wanaweza kuiletea sifa nchi yao”, alisema mwalimu huyo raia wa Japan.
Aidha alisema chama chake kimekusudia kuishawishi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhamasisha mchezo huo maskulini kwa lengo la kuwajenga watoto wa aina zote kuupenda na kuucheza.
Hata hivyo, alisema wapo wanawake wachache waliojitokeza katika mchezo huo ambao wamejipatia sifa kubwa katika mashindano ya Afrika Mashariki yaliofanyika mwaka jana, akiwataja Grace Alphonce (kg 48) na Laylat Mohammed (kg 57), walionyakua medali ya dhahabu na fedha mtawalia
No comments:
Post a Comment