Na Abdi Shamnah
UONGOZI wa Kampuni ya Leisure Hotel Changuu Island, umesema unakabiliwa na changomoto ya uharibifu wa mazingira katika eneo la bahari kuzunguuka kisiwa hicho, unaofanywa na wavuvi wazalendo, kiasi cha kutishia uhai wa rasilimali za bahari.
Uongozi huo ulitoa malalamiko hayo ulipokutana na Waziri wa Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo, Abdillah Jihad Hassan, katika ziara yake ya kukitembelea kisiwa hicho kuona maendeleo ya miradi ya utalii inayoendeshwa na Kampuni hiyo, inayomiliki Hoteli kadhaa za
kitalii hapa nchini.
Msimamizi Mkuu wa Ujenzi na Miradi Ali Saad, alisema kumekuwepo uharibifu mkubwa wa matumbawe katika eneo la bahari kuzunguuka kisiwa hicho unaotokana na mitego ya kienyeji inayotegwa na wavuvi.
Alisema mbali ya wavuvi hao kutokuheshimu kanuni inayokataza kuacha kuvua samaki katika eneo la bahari, mita 200 kuzunguka kisiwa hicho, bado wameendelea kuweka mitego katika eneo hilo na kusababisha uharibifu mkubwa wa kuvunja matumbawe na kuwafanya samaki kukosa
mahala pa kuzalia.
Alisema watalii wanaozamia katika eneo hilo wamekuwa wakilalamikia hali hiyo na kuainisha kuwa pale juhudi za haraka zisipochukuliwa, kuna uwezekano mkubwa wa matumbawe hayo kumalizika baada ya kipindi kifupi.
Aidha alisema pia kumejitokeza uharibifu wa bomba la maji linalotoka Mtoni hadi kisiwani humo, hivyo kuzorotesha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa baadhi ya nyakati.
Alisema Menejijmenti ya Hoteli hulazimika kutumia zaidi ya shilingi milioni tano kila mwezi ikiwa ni gharama za matengenezo ya bomba hilo.
Alifafanua kuwa uharibifu huo huenda ukawa unafanywa kwa makusudi kwa kuzingatia kuwa maeneo lililipopita bomba hilo ni lenye kina kidogo cha maji kiasi cha kuweza kuonekana kwa uwazi.
"Bila ya maji hakuna huduma ya Utalii hapa, tunaiomba Serikali isaidie kulipatia ufumbuzi suala hili", alisema.
Katika hatua nyingine Msimamizi huyo alisema kuna mabadiliko makubwa yaliofikiwa katika uimarishaji wa Hoteli hiyo, ili kuiwezesha kutoa huduma bora zaidi na kuvutia watalii kwa faida ya muwekezaji na Serikali.
Alibainisha kuwa hakuna vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vinavyofanyika hotelini hapo pamoja na kusisitiza azma ya kampuni kuendelea kuajiri wafanyakazi kwa kuzingatia sifa na uwezo wao bila upendeleo.
Aliuhakikishia uongozi wa Wizara kuwa Hoteli yake iko tayari kupokea wanafunzi kutoka Chuo cha Utalii kwa ajili ya mafunzo hususan wakati ule msimu unaposhamiri.
Akizungumzia mafao ya wafanyakazi, Saad alisema ni moja ya jambo muhimu linalozingatiwa na Kampuni yake kuhakikisha wafanyakazi wananufaika,hivyo huwagawia "service charge' ikiwa ni asilimia 10 ya pato lote lionalokusanywa na hoteli.
Alisema hatua hiyo inaepusha wizi mdogo mdogo wa mali za Hoteli sambamba na wafanyakazi kuwa na imani na uongozi,hivyo kuwa walinzi wa maliasili zilizopo.
Nae Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdillah Jihad Hassan aliitaka Menejment ya Hoteli hiyo kuwa na mashirikiano ya karibu na Serikali na wadau wote wa sekta ya Utalii, ili kuhakikisha hoteli hiyo inafikia lengo la kuimarisha utalii nchini.
Alisema amefurahishwa na maendeleo makubwa yaliofikiwa katika kuleta mabadiliko, yanayoifanya hoteli hiyo kuonekana kuwa mahala pazuri kwa utalii.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kulipa kodi kwa wakati na kusimamia vyema haki za wafanyakazi, ili kuondoa malalamiko.
Katika ziara hiyo Waziri Jihad alipata fursa ya kutembelea maeneo na vivutuo kadhaa vya utalii, ikiwa pamoja na hifadhi ya makobe, bwawa la kuogelea la kimaumbile,mkahawa,nyumba za kulala na gereza la kale,
Kisiwa cha Changuu (The Prisoners Island) kilikodishwa kwa Kampuni ya Leisure Hotels 2003 kwa mkataba wa miaka 33, ambapo taratibu zote za Uwekezaji zilifanyika kupitia mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).
No comments:
Post a Comment