Habari za Punde

WALIOJENGA UWANJA WA NDEGE WABANWA

Na Aboud Mahmoud

MAMLAKA ya Viwanja vya ndege Zanzibar imewataka wananchi waliojenga na wanaoendelea kujenga maeneo ya Mamlaka hiyo kusitisha ujenzi huo hadi itakapokamilisha uhakiki wa maeneo hayo.

Meneja Ufundi wa Mamlaka hiyo ambae pia ni Mkuu wa Kitengo cha Mazingira vinjwa vya Ndege, Mzee Abdallah Mzee, alitoa agizo hilo wakati wa zoezi la kuhakiki maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar mwishoni mwa wiki.


Alisema Mamlaka yake inafahamu kuna watu wengi waliojenga na wanaoendelea kujenga ndani ya eneo la Uwanja wa ndege na kuwataka wasitishe mara moja ujenzi huo.

Wananchi wengi wanadaiwa kulivamia eneo la Uwanja wa ndege ambalo lilitolewa na serikali tokea mwaka 1997 lakini kwa asilimia kubwa “limevamiwa” na kujengwa nyumba za kuishi bila ruhusa ya Mamlaka husika.

"Tunawaomba wananchi ambao wameanza ujenzi katika maeneo haya wasitishe mara moja hadi pale tutakapomaliza kufanya uhakiki wa maeneo yetu ambayo tumekabidhiwa rasmin na Serikali muda mrefu sasa,” alifafanua Meneja huyo.

Aidha, Mzee alisema Idara ya Ardhi na Upimaji ilikuwa imeweka alama za mipaka ya viwanja (Beckon) 154 kwa ajili ya kuwafahamisha watu kuwa eneo hilo ni mali ya Mamlaka lakini zimeondoshwa na kusalia nane.

"Tumeona bora tufanye uhakiki wa hili eneo kutokana na kuvamiwa na wananchi kwa ujenzi huku, Idara ya Ardhi na Upimaji ilikuwa tayari imetuekea vikuta vya alama 154 lakini vyote vimetolewa na kubakia vinane tu, alisema

Mzee alifahamisha kuwa maeneo yaliyoathirika sana na uvamizi huo ni pamoja na Chukwani, Mbuyu mnene na Mitondooni ambapo Chukwani ni hatari zaidi kwani kuna mtambo wa kuongozea ndege hasa kwa kuwa nyumba zimeezekwa mabati.

Alisema uhakiki unaofanyika utabaini nani amejenga ndani ya eneo la uwanja na yupi yuko nje, ili hatua zitakazochukuliwa zikiwemo za kuwaelimisha wananchi hao ili kupatikane muafaka.

Hata hivyo, Mzee hakusema ni muafaka wa aina gani utafikiwa endapo itabainika kuwepo nyumba ndani ya maeneo ya uwanja.


Nae Mjumbe wa Sheha kwa Shehia ya Mombasa, Hemed Ali Suleiman amesema Kamati ya Shehia yake inayoongozwa na Sheha na maofisa wa Mamlaka ya wamekubaliana kupitia eneo hilo ili kukabiliana na wanaofanya uvamizi huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.