Na Faki Mjaka Maelezo Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema imejidhatiti kikamilifu katika kukabiliana na majanga ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya uokozi katika maeneo mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Aidha imesema itaendelea kutoa elimu ya kukabiliana na maafa kwa jamii na kuimarisha kamati za maafa za Shehia, Wilaya na Taifa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Haji Omar Kheir katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kukabiliana na Maafa yatakayofanyika hapo kesho.
Amesema mikakati ambayo serikali ya Zanzibar inaifanya katika kukabiliana na majanga inatakiwa kupewa nguvu na ushiriakiano wa taasisi zote za serikali na zile za binafsi ambapo wananchi nao kwa pamoja wanatakiwa kuwajibika kwa nafasi zao.
Aidha katika taarifa hiyo Kaimu huyo amesema Serikali imedhamiria kuifanyia mapitio sheria namba 2 ya mwaka 2003 ya kukabiliana na maafa ili wieze kuendana na mahitaji na mazingira ya sasa.
Miongoni mwa mikakati ambayo pia imetajwa ni kusimamiwa kikamilifu utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kukabiliana na maafa pamoja na upatikanaji wa mawasiliano wakati wa maafa.
Sambamba na hayo Serikali pia itatafuta ushauri wa kitaalamu juu ya kuwa na mbinu madhubuti za kujikinga na maafa pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa na mafunzo kwa wadau.
Waziri Haji Kheir amesema yanapotokea majanga ulimwenguni watoto na Vijana ndio wahanga wakuu hivyo ni vyema kupatiwa elimu itakayowaweza kujikinga na majanga toka mashuleni na majumbani kupitia wazazi wao na vyonbo vya habari.
Kila ifikapo Octoba 13 ya kila mwaka ni siku ya kukabiliana na maafa duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wafanye Watoto na Vijana kuwa ni Wadau katika kukabiliana na Maafa”
No comments:
Post a Comment