Habari za Punde

MCHANGO WA AFYA UNAOTOLEWA NA CUBA KUTHAMINIWA


Makamu wa Pili wa Rais Wa Zanzibar Balozi Sei Ali Iddi akisalimiana na balozi wa cuba nchini tanzania Bw, Ernesto Gomez Diaz aliyekutana nae katika jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.


Na Othman Khamis, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema mchango wa Jamhuri ya Cuba katika kusaidia ustawishaji wa afya za wananchi wa Zanzibar, utaendelea kuheshimiwa.


Balozi Seif alieleza hayo alipokuwa akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba nchini Tanzania, Ernesto Gomez Diaz katika ofisi za Baraza la Wawakilishi huko Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema wananchi wa Zanzibar wameshuhudia juhudi zinazochukuliwa na Cuba katika kusaidia huduma za afya pamoja na utoaji mafunzo katika sekta hiyo muhimu kwa maisha ya wananchi.

Balozi Seif alisema mfumo wa mafunzo ya afya unaotolewa na wataalamu wa afya wa Cuba, umeongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi.

“Mfumo wa mafunzo ya wataalamu wa Cuba kwa watendaji wa afya wa Zanzibar umesaidia kupunguza uhaba wa madaktari ambao wengi kati yao hubakia nje ya nchi baada ya kumaliza mafunzo yao”, alisema Balozi Seif.

Makamu huyo aliishauri Cuba kuangalia uwezekano wa kuwekeza Zanzibar katika nyanja ya utalii.

Alisema Cuba tayari imeshapiga hatua kiasi katika sekta ya utalii jambo ambalo linaweza kusaidia kunyanya kipato cha wananchi kwa kuongeza ajira hasa kwa vijana.

Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania, Balozi Ernesto Gomez Diaz alisema nchi yake inakusudia kuongeza mashirikiano na mataifa ya rafiki katika kipindi kijacho.

Balozi Gomez, alisema mpango huo utazingatia zaidi nchi za Bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.