Wadai wameshindwa kumsaidia Rais
Na Mwantanga Ame
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamewashushia tuhuma nzito watendaji serikalini kwa kueleza baadhi yao hasa waliopewa dhamana ya kumsadia Rais hawawajibiki na kusababisha serikali kubebeshwa lawama isizostahiki.
Wajumbe hao walitoa kauli hizo wakati wakiujadili mswada wa sheria ya kuanzishwa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), na kuweka mazingira bora kwa ajili ya kusarifu, uendelezaji, uzalishaji biashara na ukuzaji karafuu na mazao mengine ya kilimo.
Wajumbe wa baraza hilo ambao walizungumza kwa hisia kali, waliwalalamikia baadhi ya watendaji serikalini na kudai hawako tayari kumsaidia Rais na wanatumia nafasi zao vyenginevyo.
Walisema ushahidi uko wazi kwani taasisi nyingi walizopewa kuziongoza imethibitika kuwa baadhi yao, ufanisi umeshindwa kupatikana hali inayosababisha mara kadhaa kuwataka wabadilike.
Kwa upande wake Asha Bakari Makame alisema atakuwa tayari kuwataja hadharani viongozi wasiojiweza, kwani hawawezi kulifumbia macho suala hilo kwani linaondoa imani ya wananchi kwa serikali yao.
“Baadhi ya watendaji wanaotaka kujilinda kutokana na vitendo viovu, wameanzisha mtindo wa kumpelekea Rais majina ya watu ambao wana lengo la kuwalinda huku wengine wakipeleka watoto wao ili wapewe madaraka”, alisema Mwakilishi Asha.
“Huu ni wakati wa kubadilika na sio kuendeleza kutokubali kuacha tabia ya kupeleka watoto wa shangazi kwa Rais tunampaka matope, mtu hawezi kazi aondolewe, tunamdhalilisha Rais apelekewe watu wa kumsaidia sio asukumiziwe watendaji wabovu”, alisema.
Alisema serikali Zanzibar imekuwa na wataalamu wengi, lakini hakuna kinachoonekana kufanyika zaidi ya viongozi hao kuonekana kutumia nafasi zao kujinufaisha binafsi huku utendaji serikalini ukionekana umedorora.
“Rais tusimlaumu anateua watu kwa kutambua watamsaidia tuko tayari kuwafichua watendaji hao wapo na tunawajua maana utapoyataja maovu yao basi wanakwambia wanachunguza, unaambiwa inaundwa Tume lakini inashindwa kuleta majibu ya hatua zilizochukuliwa haya tumeyaona kwa macho yetu pale tunapoyapitia Mawizara”, alisema Mwakilishi huyo.
Alisema inasikitisha kuona Zanzibar hivi sasa idadi ya watu haijafika hata milioni mbili, wakati China ina watu zaidi ya bilioni moja huku ikiweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Alisema kutokana na hali hiyo lazima uwepo utaratibu ambao utatoa kipimo cha uwajibikaji na yule asiyeweza kufikia kiwango serikali isione tabu kumuondoa.
“Lazima serikali ikubali kama wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na ni chombo kikubwa kwani wanaonekana sio lolote si chochote pale wanapotoa mawazo yao kuwataka watendaji wabadilike tumshukuru Mzee Jumbe” alisema Mwakilishi huyo.
Akizungumzia kuhusu ZSTC, alisema serikali imeamua kuandaa sheria ya kurekebisha shirika hilo, lakini bado kuna mambo yatahitajika kufanywa kwani wizara ya Biashara kuna madhambi ambayo hayasemeki yaliyoshuhudiwa na kamati.
Akitoa mfano alisema Rais wa Awamu ya tano Dk. Salmini katika kuimarisha biashara alianzisha maonesho ya biashara, lakini mwisho wa siku maeneo hayo yameachwa na kubakia mwitu huku wananchi wa Zanzibar sasa wamekuwa wakifuata maonesho Tanzania Bara.
Nae Mwakilishi wa Wete, Asaa Othman Hamad, akichangia mswada huo alisema suala la uadilifu limeshuka kwani kuna viongozi ndani ya serikali wamekuwa wadhaifu na wamekuwa wakiwakosanisha viongozi na wananchi.
Akitoa mfano alisema suala la Magendo ya karafuu kuendelea kutokea yamekuwa yakifanyika kwa kuwashirikisha viongozi wa vikosi vya KMKM kwani wanashirikiana na wavusha magendo.
“Magendo yanalindwa na vikosi vya ulinzi kwani karafuu zinapitishwa chini ya miguu ya KMKM, tunaambiwa zimekamatwa karafuu wenyewe hawakupatikana hawa wanapatana na askari wanawapa chao wanaachia karafuu, tumepoteza mwelekeo hapa”, alisema.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, alisema kuendelea kwa serikali kuingiza vipengele vya kuwa na ofisi za shirika la ZSTC nje ya nchi ni sehemu itayoifanya kutumia fedha nyingi hasa ikiwa imebainika kuwepo kwake hakuna ufanisi.
Alisema kinachohitajika ndani ya sheria hiyo ingeliweka kipengele cha kutumia mfumo wa wakala badala ya kutumia ofisi kwani wakala angeliweza kulipwa kutokana na kazi yake.
Mwakilishi wa Mtambwe, Salim Abdalla Hamad, alisema zao la karafuu linahitaji kuwekewa mazingira mazuri ikiwa ni hatua itayoweza kusaidia kukuza uchumi wa nchi.
Mapema waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, akiwasilisha mswada huo alisema, baada ya serikali kubaini kuwapo kwa matatizo katika zao hilo hasa kushuka bei imeamua kuimarisha kwa kuangalia matatizo yanayokwaza uzalishaji.
Alisema katika utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), umebainisha iwepo sheria ikiwa ni hatua itayoweza kuendesha biashara hiyo na kuhakikisha shirika linakuwa na muundo mpya ambao utapunguza gharama za uendeshaji.
No comments:
Post a Comment