Habari za Punde

CHUKI, UHASAMA HAZINA NAFASI KATIKA KULETA MAENDELEO - MAALIM SEIF

Na Khamis Haji, OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema dhamira ya ukweli katika kumaliza chuki na uhasama na badala yake kuelekeza nguvu katika kukuza maendeleo ya wananchi ndio siri kubwa ya mafanikio yanayoanza kujitokeza katika nchi za Rwanda na Zanzibar.

Maalim Seif alisema hayo jana ofisini kwake Migombani Zanzibar, alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Fatma Ndangiza aliyefika ofini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.


Maalim Seif alisema licha ya Rwanda kukumbwa na mgogoro mkubwa uliosababisha uhasama na watu wengi kupoteza maisha mnamo mwaka 1994, nchi hiyo imeweza kuchukua juhudi kubwa ya kuleta maridhiano miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo, na katika kipindi kifupi nchi hiyo hivi sasa inapigiwa mfano kwa kukuza maendeleo ya wananchi wake barani Afrika.

Makamu wa Kwanza wa Rais, alisema halikadhalika Zanzibar nayo ilikuwa ikikumbwa na migogoro mara kwa mara iliyosababisha chuki kujengeka miongoni mwa jamii, lakini baada ya wananchi wenyewe kuamua kuondokana na hali hiyo na kuwepo dhamira ya kweli katika jambo hilo, uhasama huo sasa umetoweka.

Alisema maridhiano yaliyofikiwa Zanzibar na vyama vya CCM na CUF na baadaye kupata ridhaa ya wananchi wote yamekuwa dira ya mafanikio, kwa vile hivi sasa wananchi wote wanafanya kazi kwa pamoja bila ya kujali tafauti zao, na dalili njema za mafanikio zimeanza kujitokeza.

Katika mazungumzo yao, Balozi wa Rwanda, Fatma Ndangiza alimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa Shirika la Ndege la nchi hiyo limepanga kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Kigali hadi Zanzibar.

Alisema kwamba safari hizo zitakapoanza zinatarajiwa kuinua kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii kati ya nchi mbili hizo, ambazo zote zimeweka mkazo mkubwa katika sekta hiyo, na zote mbili zina vivutio vingi vya utalii.

Balozi Fatma alisema nchi mbili hizo zinaweza kutumia fursa hiyo kufanya shughuli za utalii kwa ushirikiano wa karibu zaidi, ambapo watalii wanaoingia Rwanda wanaweza kuunganishwa kuja Zanzibar kwa kutumia fursa ya kuwepo usafiri wa uhakika na wale wanaokuja Zanzibar wanaweza kuunganishwa hadi Rwanda.

Maalim Seif, aliipongeza hatua hiyo ya kutaka kuanzishwa safari za moja kwa moja za ndege kuja Zanzibar kutoka Kigali kwa kile alichoeleza kuwa inakwenda sambamba na dhamira ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kukuza sekta ya utalii, ambayo imeonesha kuimarisha mapato kwa kiasi kikubwa.

Alieleza kwamba mazingira ya Rwanda na Zanzibar kwa kiasi kikubwa yanafanana kwa sababu zote ni nchi ndogo, hivyo hivyo hazina nafasi kubwa ya uwekezaji unaotegemea maeneo makubwa ya ardhi, na kwamba zinaweza kutumia maelewano hayo kujiimarisha katika nyanja nyengine kama vile sekta ya Teknolojia Mawasiliano na Habari (ICT).

Aliipongeza Rwanda kwa kuweza kumudu kupiga hatua kubwa katika nyanja hiyo ya ICT, na kusema Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa nchi hiyo na zaidi katika sekta hiyo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Maalim Seif alimpongeza Balozi huyo kutokana na kazi nzuri aliyofanya katika muda wake wote wa Ubalozi nchini Tanzania, na kwamba katika muda huo nchi mbili hizo ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeweza kutumia fursa kuwepo mashirikiano hayo kwa faida ya wananchi wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.