Habari za Punde

UWAJIBIKAJI, HESHIMA NJIA MBADALA KUONDOKANA NA UMASIKINI

Na Mwantanga Ame

MWANZONI mwa wiki hii baadhi ya watendaji wa serikali walimaliza mafunzo yao, nchini China juu ya Usimamizi wa Raslimali Watu.

Mafunzo haya yaliendeshwa kwa Wakurugenzi wa Utumishi Serikalini na Maafisa wa Utumishi na Mipango yakiwa na dhamira ya kuwaandaa viongozi hao kutambua umuhimu wa usimamizi wa Raslimali za nchi kwa faida ya jamii.


Hatua hiyo ya serikali ya China, ni sehemu ya kuendeleza uhusiano wake na Serikali ya Zanzibar, ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikitoa misaada mbali mbali kwa Wazanzibari ikiwemo nafasi za masomo na huduma za kijamii ikiwemo ya kiafya.

Ingawa misaada hii kwa muda mrefu ilionekana kuisaidia zaidi eneo la wataalamu wa nchi hiyo kuja hapa nchini na kushiriki na kufanya kazi kwa njia ya kutoa lakini safari hii serikali hiyo imekuja na aina mpya ya kusomesha Wazanzibar namna ya kusimamamia mambo mbali mbali ya utendaji wa shughuli za serikali katika kuhakikisha vipi wataweza kuitumikia jamii.

Mfumo huu kwa kiasi kikubwa umependwa na wengi na hasa wale ambao wamepata bahati ya kushiriki mafunzo hayo, kwani wameweza kuona jinsi serikali ya China ilivyoweza kupata mafanikio kwa vitendo na jinsi gani wananchi wake wanavyokubali mabadiliko

Hii ni kutokana na kuonekana kuwa siri kubwa ya mafanikio ya nchi hiyo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na suala la uwajibikaji na utamaduni walioujenga wa heshina kama ni sehemu ya misingi ya dini wanayoifuata katika utekelezaji wa wajibu wa kazi za serikali na mtu binafsi.

Kujengeka kwa dhana hiyo katika jamii ya watu wa Jamhuri ya China, ndio moja ya sababu kubwa ambayo imelifanya taifa hilo hivi sasa kuwa ni tishio katika uchumi wa dunia kiasi ambacho tayari baadhi ya mataifa yameanza kutaharuki na ukuwaji huo wa uchumi.

Hii inatokana na serikali ya nchi hiyo kusimamia msingi mkuu wa maendeleo ya taifa hilo kwa kuhakikisha inaifuata na kuitekeleza vilivyo sera ya maendeleo iliyojiwekea ambayo inatarajiwa ifikapo 2030 imeweza kupiga hatua iwe kwa kuyafikia maeneo mbali mbali ambayo yataweza kulet mabadiliko.

Kutokana na dhamira hiyo ya serikali ya China inaonesha wazi kuwa suala la usimamizi na utekelezaji wa sera ya maendeleo iliyojiwekea ndio msingi mkuu wa mafanikio ya maendeleo ya nchi hiyo.

Ni wazi kuwa Zanzibar ikiwa tayari imeshajifunza hilo itatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuliangalia eneo hilo kwa kuhakikisha inaapitia sera zake na kuona wapi walipokwama na mahitaji yepi yatafutwe ili kuweza kukwamuka.

Hili ni moja ya mambo ya msingi kutokana na ukweli kuwa tayari serikali imeshajiandaa na utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa 2020 ambao unakwenda sambamba na Mpango wa Kupunguza Umasikini MKUZA ambao utekelezaji wake unafanyika kwa kipindi cha miaka mitano mitano.

Ingawa mpango huu unaweza kuwa unafanana na huu wa serikali ya China, lakini utekelezaji ukawa ni wenye kutofautiana kutokana na moja kuwa nchi hiyo tayari ni yenye utajiri wa hali ya juu na hii ya Zanzibar ikiwa bado ni masikini lakini bado haipaswi kukata tamaa kama Zanzibar haiwezi kushindana na taifa hilo.

Dhana hii inapaswa isipewe nafasi katika serikali ya Zanzibar, kwani ninaamini kuwa hatua ya serikali ya China kuamua kutoa mafunzo hayo ni baada ya kuona upo uwezekano Zanzibar ikafanana na moja ya miji ya nchini kwao kwa vile tayari imekuwa na zana zinazofanana na nchi hiyo katika kuleta mabadiliko ya nchi.

Jambo la msingi ambalo serikali itapaswa kuona inalisimamia vyema ni namna ya kutumia idadi ya watu iliyonayo kwa kuwashirikisha katika kujipatia maendeleo kwa kuwajengea dhana ya kupenda kuwajibika huku wakiwapa somo la heshima dhidi ya serikali yao.

Inawezekana ikawa hilo likachukua muda kueleweka lakini haiwezekani kuendelea na dhana hiyo kwani tunaamini kuwa hivi sasa kila mwananchi anahitaji kuona anakuwa na maendeleo yake binafsi na nchi yao kwani wapo wengi ambao wamesafiri na kuona miji ya wenzao inakuwaje na maisha yanavyoendeshwa.

Kutokana na hilo ni wazi kuwa sera iliyopo itahitaji kuona inafanyiwa kazi ipasavyo yale ambayo tayari yameonekana kuwa ni njia muafaka kwa maendeleo ya Zanzibar kwa miaka hiyo ya 2020.

Hili tukiliweza ni wazi kuwa Zanzibar inaweza nayo ikawa ni mfano wa kuigwa kimaendeleo na wengi wanaweza kuja kwetu kusoma njia tulizozitumia kwa kuusimamia vyema uumini wa uwajibikaji na heshima.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.