Habari za Punde

ZANZIBAR BILA UCHAFU INAWEZEKANA - MAALIM SEIF

Ataka Manispaa, Wazanzibari wajifunze kwa mji wa Moshi
Aahidi kuibeba ZAFIAS, aifungulia milango

Na Salum Vuai, Maelezo

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ametaka jitihada za dhati zichukuliwe na kila Mzanzibari kuhakikisha mazingira ya nchi yanakuwa katika hali ya usafi.

Alisema endapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo, Zanzibar bila uchafu inawezekana.


Maalim Seif alikuwa akizungumza baada ya kusafisha mazingira ya fukwe lililoanzia pwani ya Malindi na kumalizikia katika ufukwe ulioko mkabala na hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani mjini hapa jana asubuhi.

Usafishaji huo ulioshirikisha wanachama wa vikundi mbalimbali vya mazoezi, limeandaliwa na Jumuiya ya ZAFIAS ambayo ndio mwamvuli wa vikundi hivyo, na kudhaminiwa na taasisi ya kimazingira ya Green Grant Fund yenye makao makuu yake Colorado nchini Marekani.

Maalim Seif Rais alieleza kuwa visiwa vya Zanzibar vina asili ya usafi, lakini katika miaka ya karibuni, vimekumbwa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotishia ustawi wa wananchi na vizazi vijavyo.

“Nchi yetu ni nzuri, lakini kuna kasoro kubwa, wageni wanaokuja hapa wakirudi kwao huisifia kwa uzuri huo pamoja na ukarimu wa watu wake, lakini huwaambia wenzao kuwa pamoja na hayo, Zanzibar ni chafu, kila pahala pananuka”, alifahamisha.

Alieleza, hata Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amelielezea vizuri tatizo la uchafu na kuhoji kwa nini iwe hivyo, wakati katika miaka ya nyuma nchi hii haikuwa na sifa ya uchafu kama ilivyo sasa.

Maalim Seif alifafanua kuwa, kama Wazanzibari wataamua nchi yao iwe safi, wanaweza, akitolea mfano mji wa Moshi ulioko katika mkoa wa Kilimanjaro Tanzania Bara, kwa namna wananchi na mamlaka zake walivyoamua kuung’arisha.

Alisema kwa vile Manispaa ya mji huo imelivalia njuga suala la usafi wa mazingira, na kutoa elimu kwa wananchi ambao nao wamekubali, kila mmoja katika mji huo ni askari kwa mwengine, kwani hakuna anayethubutu kutupa hata karatasi au kipande cha sigara, akitambua atakabiliwa na
adhabu ya faini.

“Wananchi wa Moshi wamehamasika kwa kuwa Manispaa imeunda kanuni ndogondogo, hata dereva wa basi akiingia katika mji huo huwakumbusha abiria wake wasitupe taka kwa madirishani, kwani hata basi
litaadhibiwa.

“Kilichowahamasisha watu wa Moshi ni kwamba anayekamatwa akichafua mji hutozwa faini ya shilingi 50,000 hapo hapo, na nusu ya fedha hizo huenda kwa mkamataji au aliyetoa habari, kwa nini Zanzibar hatuwezi kufuata mfano huo?”, alihoji Makamu wa Kwanza wa Rais.

Kwa upande mwengine, alisema utashi wa binadamu umechangia sana kuharibu mazingira ya bahari na ardhi, kwa kuhujumu matumbawe na kusababisha kupungua kwa samaki, pamoja na kukata miti na hivyo kuwa chanzo cha uhaba wa mvua nchini.

Aliwashangaa wavuvi wanaovua bila kufuata taratibu kwa kuharibu mazalia ya samaki, na baadae kulalamika kuwa katika maji madogo hakuna tena samaki, akihoji ni vipi watabaki wakati nyumba zao zimeharibiwa.

Alisisitiza kuwa ni lazima Wazanzibari wabadilike, na kutaka Baraza la Manispaa liisaidie serikali katika kutoa elimu kwa umma na kuandaa pamoja na kutekeleza kanuni zitakazowafanya wananchi waelewe na kusimamia suala.

Alikosoa tabia iliyojengeka kwa watendaji wa taasisi za umma nabinafsi, kuwa hodari wa kuunda mikakati na sheria, lakini zikashindwakuzisimamia na kubaki kuota vumbi ndani ya makabati, na kusema kuoneana muhali ni tatizo kubwa linalokwamisha utekelezaji wa sheria hizo.

Aliishukuru jumuiya ya ZAFIAS kwa uamuzi wake wa kujishughulisha na mambo yenye manufaa kwa jamii ikiwemo usafi wa mazingira, kufanya mazoezi kwa kujenga afya pamoja na mapambano dhidi ya maradhi ya UKIMWI.

Aidha aliishukuru taasisi ya Green Grant Fund kwa kuunga mkono na kuwezesha zoezi hilo na kumuomba mwakilishi wake Janet Awimbo, kuzidisha ushirikiano na jumuiya kama hizo hapa nchini, ili kuweza kuibadilisha Zanzibar na kuifanya kivutio cha utalii kutokana na usafi.

Maalim Seif aliwaahidi wanachama wa ZAFIAS kuwa, serikali itahakikisha ombi lao la kupatiwa sehemu ya kujenga kituo na kiwanja cha mazoezi pamoja na ofisi, linapatiwa ufunguzi kama walivyoomba na kuahidiwa mwaka jana, wakati jumuiya hiyo ilipozinduliwa na aliyekuwa Waziri
Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, ambapo jana walikumbushia kupitia risala yao.

Mapema, Mwakilishi wa Green Grant Fund Janet Awimbo, alisema kuhudhuria kwa Makamu wa Rais katika shughuli hiyo adhimu, kunaonesha ni namna gani Serikali ya Zanzibar inajali na kuthamini juhudi za kutunza mazingira.

Akieleza namna alivyovutiwa na mpango mzima wa zoezi hilo, alisema salamu za Wazanzibari katika mambo ya usafi, zitafika katika ofisi yake Colorado, akiamini kuwa zitaishawishi taasisi hiyo kuendelea kudhamini harakati kama hizo hapa nchini.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis, aliwasifu wanachama wa ZAFIAS kwa kuwa ni watu wasafi wa fikra, vitendo na utekelezaji wa maazimio yao, na baadae kumtunukia Makamu wa Kwanza wa Rais uanachama wa heshima wa jumuiya hiyo, ambao
aliukubali.

Zoezi hilo la kusafisha fukwe lilianzia Malindi pembezoni mwa mkahawa wa Mercury pamoja na Mbweni Zanzibar Beach Resort, pwani ya Kizingo, Mazizini, Ngazimia na hatimaye wanachama kukusanyika katika ufukwe huo mkabala na hoteli ya Zanzibar Ocean View

2 comments:

  1. Kwa vyovyote vile, Moshi haiwezi kufananishwa na mji wa ZNZ katika suala la usafi kwa sababu zifuatazo:
    1) Kule watu wameenda skuli sana, halafu wanaamini walichokisoma.
    2)Mchagga hana muhali na mtu hata awe ndugu yake (Uyakhe marufuku!)
    3)Pamoja na kwamba Moshi sio kubwa kijorafia,lkn. watu wengi hawajuani.
    4)Kubwa zaidi, Mji wa moshi unadhibitiwa na wenyeji(Hamna wahindi, Warabu n.k.) na wenyeji wengi hawapendi kuishi mjini, ikifika jioni karibia mji wote mtupu! wikiendi ndio kabisa (watu wako mashambani) hivyo ni rahisi kudumisha usafi.

    ReplyDelete
  2. wewe unapenda uchafu vundo

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.