Habari za Punde

ZANZIBAR IMEJISUKA UPYA KISIASA

Na Ramadhan Makame

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema huku Tanganyika ikisherekea miaka 50 ya Uhuru, Zanzibar kwa upande wake ina mengi ya kujivunia hasa baada ya kujisuka upya kisiasa.

Alisema mitafaruku na kutoelewa kutokana na hitilafu za kisiasa miongoni mwa Wazanzibari kumetoweka baada wananchi kuridhia muundo wa serikali ya Mapinduzi yenye Umoja wa Kitaifa.


Balozi Seif alieleza hayo katika hoteli ya Tembo iliyopo mjini hapa, kwenye hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa ajili ya Mabalozi wa nchi zote za nje wanaoziwakilisha nchi hizo Tanzania.

Balozi Seif aliwaeleza Mabalozi hao kuwa chini ya mfumo huo, Wazanzibari wamekuwa wakifaidika na matunda ya kuishi kwa umoja, amani na kushirikiana katika ujenzi wa nchi yao.

“Mfumo huu wa kuunda serikali ya Umoja, umekuwa wa manufaa sana kwa wananchi, wanaishi pamoja wanashirikiana na kufanyakazi pamoja, siasa zile la ndugu kufarikiana hazipo, hili ni jambo la kujivunia sana”, Balozi Seif aliwaeleza Mabalozi hao.

Aidha alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na kuzidisha ushirikiano baina yake na nchi marafiki na kuwaeleza Mabalozi hao kwa wakati wowote wanakaribishwa Zanzibar.

Kwa upande wake waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema nchi zenye matatizo na migogoro ya kisiasa pahala pazuri pa kuja kujifunza jinsi ya kuondokana na matatizo hayo ni Zanzibar.

“Kama yapo mataifa yana matatizo ya kisiasa na hitilafu baina yao, pahali pekee pa kuja kujifunza namna ya kuepukana na matatizo hayo ni Zanzibar, Wazanzibari wanaishi kwa amani baada ya kukaa pamoja na kuzika tofauti zao”,alisema waziri Membe.

Waziri Membe alisema Tanzania imeamua kufanyia ziara mabalozi hao ikiwa ni maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika, kutembelea sehemu mbali mbali zenye historia.

Alisema nafasi waliyoipata Mabalozi hao ya kutembelea Butiama alipozikwa Mwalimu Julius Nyerere na Kisiwandui alipozikwa Hayati Abeid Amani Karume, ni kielelezo kwa Watanzania wanawaenezi kiuhalisia viongozi hao waliotoa mchango mkubwa kwenye uhuru na ujenzi wa Muungano.

“Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume ni viongozi wa mfano wa kuigwa kutokana na amani na kujitolea kwao katika kupigania uhuru ambapo leo hii tunafurahia matunda yao”,alisema waziri Membe.

Naye kiongozi wa msafara wa Mabalozi hao, Balozi Juma Khalfan Mpango alisema ujio wa jopo la mabalozi hao Zanzibar utafungua ukurasa mpya wa mashirikiano baina ya nchi hizo na Zanzibar.

Balozi Mpango alisema ziara ya Mabalozi hao itazidisha ushirikiano na urafiki baina ya nchi hizo na Zanzibar.

Katika zaira hiyo Mabalozi hao walitembelea Butiyama, mbuga za Serengeti, Ngorongoro na kumalizikia Zanzibar ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.