Habari za Punde

BUSARA YAZIDI KUPANDA CHATI

Na Mwandishi Wetu

WAKATI taasisi ya 'Busara Promotions' ikijiandaa na tamasha la Sauti za Busara mwezi Februari mwakani, idadi ya watu wanaotembelea tovuti ya taasisi hiyo imeongezeka maradufu.

Kuongezeka huko kunadhihirisha umaarufu wa tamasha hilo linalofanyika kila mwaka, ambapo wasanii wa muziki kutoka nchi mbalimbali duniani hushiriki kuonesha kazi zao.


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa, katika mwezi huu wa Novemba, watu 1,712,190 waliitembelea tovuti ya Busara, idadi ambayo ni sawa na watu 57.073 kwa siku.

Nchi zinazoongoza kwa watu wao kutafuta taarifa za taasisi hiyo kwa mpangilio, ni Marekani, Afrika Kusini, Visiwa vya Carribean, Tanzania, Poland, Kenya, Denmark na Sweden.

Nyengine ni India, Ujerumani, Russia, Italia, Uingereza, Ufaransa, Norway, Hispania, Japan, Uholanzi, Australia, Ureno, Canada, Uswisi, New Zealand na Uganda.

Muasisi na Mwenyekiti wa 'Busara Promotions', Simai Mohammed Said, alipoulizwa juu ya mafanikio ya tamasha la Sauti za Busara linalotimiza miaka minane mwakani, alisema limekuwa kiunganishi na balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar kupitia tasnia ya muziki na hivyo kuongeza idadi ya watalii nchini.

"Ni ukweli usiofichika kwamba tamasha letu limeweza kuwaunganisha pia wasanii wa nchini na wenzao wa kimataifa, katika kukuza utamaduni ambapo watalii wengi wamevutika kuja hapa na hivyo kuongeza pato la wasanii na taifa kwa jumla", alifafanua.

Aidha, alisema wageni wanaokuja hawaishii kuangalia tamasha pekee, bali pia hutembelea vivutio mbalimbali vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama Tanzania Bara, na hivyo kuzinufaisha nchi zote mbili zinazounda muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.