WAJUMBE wa kamati ya hifadhi ya mtoto kisiwani Pemba, wamelaani vitendo vinavyoendelea kufanyika vya kuwauzia na kuwashirikisha watoto katika biashara ya dawa za kulevya.
Kauli hiyo waliitoa huko Gombani katika ukumbi wa Idara ya ustawi wa jamii Chake Chake, mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wajumbe wa katika kikao cha kamati hiyo.
Wajumbe hao walisema kuwa, vitendo hivyo ni hatari sana kwa watoto na ni kinyume na maadili ya kizanzibari, sambamba na kupoteza nguvu kazi ya taifa ambayo ndiyo tegemeo la nchi hapo baadae.
Walifahamisha kuwa, kwa sasa wanaouza dawa hizo wamebuni njia mbali mbali za kuuzia dawa hizo, ikiwemo ya kuichanganya na uji, kufanya kashata, keki, ambapo kwa ghafla mtu hawezi kujua ni kitugani.
Wakizungumzia suala la kuingiliwa na watu 11 kwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 10 huko Shumba Viamboni, Wilaya ya Micheweni, wamesema kuwa suala hilo ni la unyanyasaji, kinyama na wala halifai katika jamii kwa mtoto mdogo kufanyiwa tendo kama hilo.
Aidha wajumbe hao, waliitaka serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuchukua za kuwalinda na kuwahifadhi, kuwanusuru na matatizo mbali mbali yanayoweza kuwapata, na kutilia mkazo kwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao 11, waliomuingilia mtoto huyo.
Mmoja ya wajumbe hao, Ahmed Rashid, aliitaka kamati hiyo ya hifadhi ya mtoto Pemba, kutokusubiri kutibu badala yake kwanza kutoa elimu juu ya udhalilishaji wa watoto kwa jamii huku wakiendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa ili vitendo hivyo viweze kupungua kabisa nchini.
Alisema kuwa, pindi jamii ikipatiwa elimu ya kutosha hususana vijijini, basi jamii hiyo inaweza kupunguza na hata suala hilo kuondoka kabisa pindi watakapo elimishwa wazazi na watoto wao, ili kuweza kuwakinga watoto kuingia katika vitendo vya udhalilishaji.
Hata hivyo, Ahmed aliitaka jamii kurudisha malezi ya pamoja kwa watoto, sambamba na vyombo vya sheria kuharakisha kesi za udhalilishaji hazibakii katika vituo vya polisi na badala yake zinapel;ekwa mahakamanina watuhumiwa kutiwa hatiani.
No comments:
Post a Comment