Habari za Punde

MSALABA MWEKUNDU KUENDELEA KUSAIDIA JAMII

Na Fatma Kassim, Maelezo

CHAMA cha Msalaba mwekundu Tanzania kimesema kitaendeleza misaada yake ya kijamii kwa Zanzibar ikiwa ni hatua ya kuimarisha utoaji wa huduma mbali mbali ikiwemo maji safi na salama.

Hayo yamebainika kufuatia ziara maalum iliyofanywa Chama cha msalaba mwekundu ya kutembelea miradi mbali mbali iliyochini ya chama hicho kwa ufadhili wa Chama cha Msalaba mwekundu cha Ujerumani hapa Unguja.


Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Chama hicho Raymond Kanyombo alisema lengo la kufanya ziara hiyo hapa Zanzibar ni kuangalia miradi iliyo chini ya chama hicho na kuweza kufahamu changamoto zinazoikabili miradi hiyo.

Alifahamisha kuwa miradi mbali mbali imetekelezwa hapa Zanzibar ikiwa na pamoja na kujenga jumla ya visima 300 kwa visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kujenga majengo makubwa ya Ofisi ya Chama hicho yaliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 200.

Aliwataka wananchi waliobahatika kufikiwa na miradi hiyo katika vijiji vyao wafahamu kuwa miradi ni yao, hivyo matatizo yanapojitokeza wasisite kufanya matengenezo kwa mashirikiano ya pamoja ili huduma ziweze kunufaisha jamii.

Alisema chama cha Msalaba mwekundu kitaendelea kutekeleza miradi mbali mbali ya kijamii kwa maeneo ambayo hayajafikiwa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Nao wananchi wa vijiji vya Kikungwi na Cheju Zuiyani, walisema wana furaha kupata maji safi na salama katika vijiji vyao kupitia chama cha msalaba mwekundu ambapo hapo awali walikuwa wakikosa huduma hiyo.

Hata hivyo walisema mara nyingi ilikuwa ikiwalazimu kutembea nusu meli kufata huduma ya maji jambo ambalo lilikuwa linakwamisha shughuli nyengine za kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.