Na Mwantanga Ame
NDOTO za Zanzibar kuwa na chanzo chake cha nishati ya umeme zinaweza kutimia baada ya kampuni ya ‘Indomount’ ya nchini India kuwa na mipango ya kuwekeza katika sekta hiyo visiwani hapa.
Uongozi wa kampuni hiyo umekutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Mjini Dodoma kwa lengo la kuelezea nia yao ya kutaka kuwekeza nishati hiyo visiwani Zanzibar.
Meneja mkuu wa Kampuni hiyo Dk. Sudhakar K. alieleza kuwa wameichagua Zanzibar kuwekeza mradi huo ikiwa ni hatua ya kampuni hiyo kuona inashiriki kukuza maendeleo ya Zanzibar.
Alisema nishati ya umeme unaozalishwa kwa kutumia upepo upo uwezekno mkubwa kwa Zanzibar kuweza kufaidika nayo kwani tayari zipo baadhi ya nchi za Afrika wamekuwa wakizalisha huduma hiyo kwa njia ya upepo.
Alisema endapo serikali itakubali kuwekeza utoaji wa huduma ya umeme kwa kutumia upepo, inakusudia ndani ya kipindi cha miezi 12 itakuwa imekamilisha kufanya uchambuzi yakinifu wa mradi huo ambapo uwekezaji utaanza rasmi baada ya kukamilika kwa kazi hiyo.
Alisema suala la msingi ambalo hivi sasa wanaliangalia ni namna ya kuweza kuyapita baadhi ya maeneo ambayo yataweza kufaa na kuyatumia kwa ajili ya kuzalisha mradi huo.
Alisema wanalazimika kufanya hivyo kutokana na kuangalia hali halisi ya mahitaji ya wananchi pamoja na serikali kwa kuzingatia umuhimu wa nishati hiyo wapi itaweza kufanya kazi vizuri na kuwaletea maendeleo na maisha bora.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, aliishukuru kampuni hiyo kwa kuitikia wito wa kutaka kuwekeza katika sekta hiyo kwani kwa muda mrefu serikali imekuwa ikiwaomba wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika sekta hiyo muhimu na yenye mchango mkubwa kwa maendeleo.
Alisema kitendo cha kampuni hiyo kuichagua Zanzibar kuwekeza mradi huo ni mwanzo mzuri ambao serikali itahakikisha inauzingatia uchambuzi ambao wataufanya kwa ajili ya mradi huo.
Alisema suala la umeme visiwani Zanzibar hivi sasa upo katika hali inayotaka usaidizi kwa kuwa na vyanzo mbadala zaidi ikiwa ni hatua itayoweza kuisaidia jamii katika sekta mbali mbali hasa ya maeneo ya uzalishaji.
Wawekezaji hao pia walieleza dhamira yao kuona wanaingia katika sekta tofauti ikiwemo ya uzalishaji wa samaki kwa kuvua katika bahari kuu.

No comments:
Post a Comment