Asema wahisani wamechoka, waanza kuweka masharti ya ajabu
Na Salum Vuai, Maelezo
WAZANZIBARI wana kila sababu ya kuhakikisha Tamasha la Sauti za Busara linadumu na halihami kwa sababu za kukosa ufadhili kutokana na umuhimu wake katika utalii unaotegemewa kwa kuimarisha uchumi wa nchi.
Hayo yamesemwa jana na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akifungua mkutano wa siku moja kati ya wadau wa sekta ya utalii, na viongozi wa taasisi za biashara na uchumi katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Mkutano huo uliandaliwa na taasisi ya Sauti za Busara kwa lengo la kuelezea umuhimu wa tamasha hilo pamoja na mengine kwa kukuza uchumi wa Zanzibar ambapo washiriki walichangia njia mbalimbali za kuyafanya matamasha kuwa endelevu na yenye tija kwa jamii.
Maalim Seif alisema hakuna shaka kwamba matamasha ya utamaduni na muziki yana mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi kwa vile yanapofanyika huvuta watu mbalimbali kutoka nchi za nje, ambao huingiza fedha nyingi kupitia sekta ya utalii.
Alifahamisha kuwa, katika kipindi cha mwezi Februari linapofanyika tamasha la Busara hapa nchini, athari zake kwa uchumi wa nchi huonekana waziwazi kutokana na kuongezeka kwa harakati za kibiashara kwa taasisi, kampuni na hata watu mmoja mmoja.
"Ushahidi huo unatoa njia kwa sote tuliokusanyika hapa kufahamu nafasi ya utamaduni kama nyenzo ya kuleta ufanisi kwa wananchi wa Zanzibar na mustakbali wa uchumi wa visiwa vyetu, Sisi Wazanzibari tunajivunia tamaduni zetu, lugha, historia, vyakula, mavazi pamoja na utajiri wa muziki wa asili", alieleza Makamu wa Kwanza wa Rais.
"Muziki hususan, ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Unatuunganisha katika matukio mbalimbali ya kijamii. Ni kielelezo kinachoonesha sisi ni nani na tunataka tuwe nani", alisema akikariri maneno ya Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.
Alisema tishio la uwezekano wa tamasha la Busara mwaka 2012 kuwa la mwisho na kufikiria kulihamishia nje ya Zanzibar kutokana na gharama kubwa za kuliendesha, lisipewe nafasi kutokea, kwani dunia haitawaelewa waanzilishi wake na Wazanzibari kwa jumla.
Aliwataka Wazanzibari wote kuelewa kuwa tamasha hilo ni lao, na kwamba iko haja sasa kwa makampuni ya ndani, taasisi zinazonufaika na ujio wa watalii wanaohudhuria matamasha nao kuchangia gharama hizo ili kuwapunguzia mzigo waandaaji wake.
Alisema tamasha hilo ni kubwa, na kwamba tayari limekuwa maarufu na kuwekwa katika kalenda za kimataifa, hivyo si vyema likaondoka hapa kwa sababu ya kukosa ufadhili.
Alikiri kuwa wafadhili hao wamechoka kubeba, kiasi cha kuanza kuweka masharti magumu kutekeleza kabla kutoa fedha zao, hivyo ni lazima sasa Wazanzibari wajipange kuacha kutegemea mbeleko za wahisani.
Alieleza kufurahishwa kwake kwa kuwepo taasisi mbalimbali za utamaduni hapa nchini, kama vile 'Busara Promotions', Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi (DCMA), ZIFF, Jahazi na ile iliyoanzishwa hivi karibuni, 'Swahili Performing Arts', ambazo alisema zinafanya kazi kubwa kukuza sanaa na utamaduni wa visiwa hivi.
Aidha alisema Serikali ya Zanzibar inasaidia kuimarisha matamasha likiwemo Mwaka Kogwa, pamoja na Utamaduni wa Mzanzibari yanayofanyika kila mwaka ambayo pia huvutia watalii wengi na hivyo kukuza pato la taifa.
Akimkariri Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein wakati akifungua tamasha la Sauti za Busara mwaka huu, alisema kuwa tamasha hilo ni njia ya ajira, alieleza matumaini yake kuwa, vyote kwa pamoja, uwekezaji na kukua kwa ubunifu, utalii wa kiutamaduni, jitihada za serikali na utulivu wa kisiasa uliopo nchini, vitasaidia vita vya kumaliza umasikini kuelekea lengo la milenia na dira ya Zanzibar 2020 chini ya mkakati wa kupambana na umasikini, MKUZA.
Akizungumzia haja kwa wafanyabiashara wazalendo pamoja na taasisi mbalimbali zilizopo nchini kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu kuliendesha tamasha la Sauti za Busara na mengine, Maalim Seif alisema haitakuwa vyema kuendelea kuwa tegemezi kwa kuachia taasisi za kigeni pekee kuyabeba matamasha hayo.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema ushahidi unaonesha kuwa, matamasha yana sehemu muhimu ya kuendeleza amani na utulivu katika ukanda huu, katika kujenga heshima kwa tamaduni mchanganyiko, kutambua na kufahamu umuhimu wa nyanja hiyo.
Kwa upande mwengine, alisema matamasha hayo yanaweza kutumiwa katika kuwaunganisha watu wa Afrika Mashariki na kujenga maelewano mazuri miongoni mwao, kwa kuimarisha njia ya kuunda shirikisho lao.
Mapema, Mkurugenzi wa 'Busara Promotions' Yussuf Mahmoud, alisema kwa miaka kadhaa sasa, tamasha hilo linasifika ulimwenguni kote kwa kuwaunganisha wasanii wa ndani a wale wa kimataifa, pamoja na kutoa fursa kwao ya kujifunza muziki kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na kuutambulisha muziki wa Afrika Mashariki kwa wageni.
Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake kuwa tamasha la mwakani litakuwa la mwisho kufanya hapa Zanzibar na kufikiria uwezekano wa kulihamishia nje ya visiwa hivi, kutokana na waandaaji wake kuelemewa na gharama kubwa za uendeshaji na ugumu wa kupata ufadhili.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wa kwanza wa aina yake, walishauri serikali iandae utaratibu wa kuwatoza asilimia ya faida, wawekezaji wa hoteli za kitalii na wafanyabiashara wengine ambao kwa njia tafauti hufaidika na ujio wa watu wanaokuja kuhudhuria matamasha hayo.
Aidha walitaka kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa utamaduni, wazo ambalo Makamu wa Rais aliahidi kuliwasilisha serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment