Yatamani kukutana na Kilimanjaro Stars mbele ya safari
Na Salum Vuai, Maelezo
PAMOJA na wachezaji wa timu ya taifa ya soka 'The Zanzibar Heroes' walioko kambini nchini Misri kusikitishwa sana kwa kutowasili kwa wenzao waliokuwa na Taifa Stars, hali hiyo imeelezewa kuwaongezea ari ya kudhihirisha nia yao ya kunyakua ubingwa wa Chalenji mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana kutokea jijini Cairo, Msaidizi Katibu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Masoud Attai, alisema kutokana na kitendo hicho ambacho wanaamini imefanywa makusudi ili kuhujumu timu hiyo, wachezaji wa Zanzibar Heroes wameahidi kuwa, hawataangusha Wazanzibari wakati wa michuano hiyo.
"Ni kweli kushindwa kuja kwa Cannavaro na wenzake, kumechangia kushusha morali wa wachezaji walioko huku, lakini tumechukua juhudi kuwahamasisha, wametulia na pia nasaha za Waziri Jihad na Balozi Shauri, zimesaidia kuwarejesha katika ari", alisema Attai katika mazungumzo na gazeti hili.
Alieleza kuwa, wachezaji wote pamoja na makocha walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa ujio wa wanandinga hao mahiri na wazoefu, ili wapate angalau mazoezi ya siku chache kabla kuondoka huko, mithili ya wanajeshi walioko mpakani wanavyosubiri kupata mizinga.
Zanzibar Leo pia iliweza kuzungumza na kocha Abdelfatah Abbas, Mmisri anayesaidiana na Hemed Moroko, ambaye alisema vijana hao wameonesha mwelekeo wa ufahamu na kushika vyema maelekezo wanayopewa.
"Kufungwa katika mchezo wa majaribio wa awali 2-0 juzi 3-0, kulitokana na vijana kutozoea hali ya baridi na mapengo ya akina Aggrey Morris, lakini tunaamini watakomaa na kufanya vizuri katika mashindano Dar", alisema Abbas.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Othman Omar Tamim 'Mani', alieleza kuwa ingawa timu yao haikupangwa na ndugu zao wa Kilimanjaro Stars katika hatua ya makundi, lakini wanatamani wakutane nao mbele ya safari kwani mchezo kati ya timu hizo unafahamika kama fainali ya mashindano.
Alieleza kuwa, wachezaji wote wako katika hali nzuri na ari ya kuwasili Dar es Salaam ili wafanye kile kinachotarajiwa na Wazanzibari, ingawa kuna dalili za kuanza kuhujumiwa mapema na baadhi ya wapinzani wao, hasa kwa sakata la kukaliwa paspoti za wachezaji watatu wa timu hiyo na kukosa viza za safari.
Wanandinga waliokwama kusafiri juzi kwa kile kilichoelezwa paspoti zao kung'ang'aniwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo lilichukua dhamana ya kuzigonga viza, ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Aggey Morris na Mwadini Ali, pamoja na Nassor Masoud ambaye ingawa alikuwa amekamilisha taratibu nyengine za safari lakini alikosa kadi ya chanjo ilidaiwa kushikiliwa na daktari wa klabu anayoichezea Simba.
Aidha kocha mkuu wa timu hiyo Stewart John Hall, alishindwa kundoka kwa kujaa paspoti yake, hali iliyosababisha akose viza ya Cairo.
No comments:
Post a Comment