Na Mwashamba Juma
WAZIRI wa Maji Ardhi Makaazi Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna, amesema mradi wa kuyachakachua maji ya bahari hadi kunywewa bila ya chumvi, ni wa aina yake kuanzishwa katika historia ya Zanzibar.
Alisema mradi huo ambao utawanufaisha kiasi cha wananchi 600 wa kijiji cha Chwaka, ni miongoni mwa jitihada za serikali katika kuwapunguzia dhiki ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Shamuhuna alieleza hayo alipokuwa akizundua mradi huo, uliofadhiliwa na serikali ya Ujerumani kupitia kampuni za Mork Water Solution na Dow Chemicals.
Alifahamisha kuwa mradi huo ni mafanikio makubwa kwenye harakati mpango wa kupunguza umasikini na kuyafikia malengo ya milenia.
“Maradi huu tunaouzindua ni ukurasa mpya katika historia ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Ujerumani, sio tu wa ajabu, lakini pia ni wa kwanza kuanzishwa visiwani hapa”, alisema Shamuhuna.
Alisema juhudi za kuyabadilisha maji ya bahari kuwa maji safi na salama ni juhudi ambazo zinafaa kushukuriwa na kupongezwa kwa sana.
Nae kiongozi wa mradi wa Mork Water Solution, Puy alisema waligundua kwa muda mfupi tu wazo la kubadilisha maji safi na salama yanayotokana na maji ya bahari.
Alisema mradi huu wa mwanzo kwa visiwa vya Zanzibar ukiwa na lengo la kufikisha maeneo mengine zaidi vijijini hasa vile vyenye matatizo ya maji ya chumvi katika maeneo ya pwani.
Alishukuru mashirikiano aliyoyapata kutoka kwa watu waliojituma usiku na mchana katika kufanikisha mradi huo na kuhakikisha wakaazi wa Chwaka wanapata maji safi na salama.
Naye Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Brandes, alisema matatizo ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa vjiji vya Chwaka ni miongoni mwa sababu iliyoifanya Ujerumani kusaidia mradi huo, na kwa ushahidi wa mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Zanzibar na Ujerumani.
“Tumeanzisha mradi huu, hadi hapa tulipofikia na tutaendelea kuleta miradi mingi zaidi, narudia kusema maji safi kwa wote”, alisema Balozi huyo.
Mradi umegharimu zaidi ya Euro 409,000, ambapo serikali ya Ujerumani imechangia Euro 176,000, Mork Water Solution imechangia Euro 183,000 na kampuni ya DOW imechangia Euro 50,000.
Katika maradi huo kisima kimechimbwa katika Chuo cha Usimamizi wa fedha cha Chwaka, ambapo kimefungwa mashine ya kuchuja maji hayo badala ya kuwa ya chumvi huwa safi yenye kufaa kunywa na matumizi mengine.
No comments:
Post a Comment