Serikali yaombwa kuchunguza misaada
Wabunge Zanzibar wailaani CHADEMA
Na Mwantanga Ame, Dodoma
BAADHI ya wabunge wamehusisha mabalozi, nchi na mashirika ya kimataifa katika kujihusisha kuingilia mchakato wa upatikanaji wa katiba nchini Tanzania.
Mchakato huo hivi sasa uko bungeni ukijadiliwa katika hatua ya awali ya kupatikana kwa sheria itakatoa mamlaka ya kuundwa kwa tume itakayoratibu ukusanyaji wa maoni ya wananchi.
Wakijadili mchakato huo, wabunge hao walisema baadhi ya mataifa ya nje yanatia mikono na kuchangia kuuvuruga mchakato huo kwa kukisaidia chama cha CHADEMA na makundi ya wanaojiita wanaharakati.
Wakichangia mjadala huo, wabunge hao walisema ipo hofu kubwa kuwa CHADEMA, kimejitoa kwenye mjadala huo Bungeni kutokana na kushindikizwa na nchi zinazokifadhili chama hicho.
Wakati wabunge wakijadili na kuzishushia lawama nchi hizo, ndani ya ukumbi wa Bunge, Balozi wa Marekani na Norway, wanaoziwakilisha nchi zao waliweza kuzisikia wazi wazi shutuma hizo kupitia wakalimali wa ndani ya Bunge hilo.
Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa, alisema Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, wanapaswa kufanya majukumu yao yaliyowaleta na si kuingilia mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya ya Tanzania hauwahusu.
Alisema haitakuwa busara kuona kunakuwa na hujuma kwa ajili ya mswaada huo kutoka kwa mabalozi kwa kuusaidia upinzani na kama mabalozi wana utaratibu wa kusaidia vyama ni vyema basi wakafikiria kukaa na CCM ndio yenye serikali na sio vyama vyengine.
Alisema Tanzania ni nchi iliyojitawala na imekuwa na uhuru wa kufanya mambo yake kwa vile ni nchi inayojitawala na hatiapendeza kuona mabalozi wanakuwa ni vinara kuleta machafuko nchini.
Alisema Tanzania inajua wapi inapotaka na wapi inakoelekea, hivyo ni lazima watumie Bunge kupanga wanapotaka kwenda na Watanzania wasikubali kupotoshwa na watu walio nje ya nchi.
Nae Mbunge wa Jimbo la Urugu, Mkoa wa Singida, Mwiguru Mchemba, alisema inaonekana kuna watu wanapanda farasi wawili, lakini watambue hawawezi kwenda katika mfumo huo katika mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania.
Alisema hivi sasa kuna taarifa za kuwa tayari kuna makundi yameanza kupokea fedha za misaada na haitambuliki walipewa kwa kutumia masharti gani, lakini wahahakikishe isipopatikana katiba wajue sio CCM itayokuwa haina katiba bali ni watanzania walikosa kuwa na katiba.
Na Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda alisema serikali inapaswa kufanya uchunguzi dhidi ya watu wanaotumiwa kuuchafua mchakato wa katiba, kwani inaonekana hivi sasa kuna baadhi ya misaada ghasi inayotolewa kwa ajili ya kuhujumu mjadala wa katiba uvurugike.
Alisema kuna watu hivi sasa wameamua kupaza sauti wanategemea wafadhili kwa kutumia suala la mabadiliko ya katiba na ipo haja ya serikali kufanya uchunguzi kuona wanaowafadhili ni watu wa aina gani.
“Wanaolipa mpiga zumari wanafaidika na nyimbo waitakayo na tayari kuna watu katika nchi za Afrika wanaingilia mjadala hii na imekuwa kuna baadhi ya watu kuchochea na kuleta mifarakano ushawishi upo na tusikubali kuona kuna matakwa ya mtu ama nchi ” , alisema Mbunge huyo.
Kwa upande wake, Injinia Stela Manyanya alisema suala la katiba linapaswa kutambua kuwa hakuna mtu wala kikundi chochote kitachoachiwa kuvuruga suala hilo kwa kuona wachwe mjadala huo ni wa watu au kundi fulani.
Alisema inasikitisha kwa CHADEMA kudai baadhi ya maeneo wananchi walihusika kuwashauri kuwa hawakubaliani na mswada huo wakati hata kuonekana katika wilaya ikiwemo anayoiongoza yeye hawakufika.
Alisema inashangaza kuona kuna NGO’s kudai kuwa zimepata maoni ya wananchi juu ya hilo wakati hazijawahi kuonekana katika mikoa wanayoiongoza huku kuna mashirika ya maendeleo ya kimataifa na
wanaharakati wakitumia nafasi hiyo kupotosha mswada huo kupitia ufadhili wa mataifa ya nje.
Mbunge wa Kikwajuni, Masauni Yussuf, akitoa mchango wake alieleza hali ya dharau kwa Zanzibar inayoendelea kutolewa na Mbunge wa CHADEMA Tundu Lisu, imeonekana hivi sasa kuzoeleka jambo ambalo wazanzibari hawawezi kuona inakivumilia kitendo hicho.
Mbunge huyo alisema ili kukomesha dharau hiyo bado Mbunge huyo anayo nafasi ya kuona anatumia nafasi hiyo kuwaomba radhi Wazanzibari kutokana na maneno yake aliyotoa ni ya dharau kwa Zanzibar.
Nae Mbunge wa Jimbo la Magomeni Mohammed Chombo, alisema kuna mambo yanayoonekana kutia wasi wasi kama Lissu anahaja kuwepo kwa Muungano wa Tanzania, kutokana na hotuba zake zote katika Bunge kuonyesha viashiria vya kutaka kuvunja muungano kwa gharama yoyote na haijulikani ametumwa na nani.
Alisema matamshi ya Lissu, hivi sasa ni sawa na nyimbo za rusha roho kwani hujaaa maneno ya kashfa na matusi na atambue anachokifanya ni sawa anaimba rusha roho kiasi ambacho anatia uchungu ndani ya nafsi za Wazanzibari.
Hata hivyo, Mbunge huyo aliwataka Wazanzibari kuona wanatulia na waweze kutoa maoni yao ili kuhakikisha Muungano unadumishwa kwani hadi sasa maandalizi yaliofanyika yamewashirikisha serikali katika hatua zote.
Alisema inasikitisha kuona Mbunge huyo amekuwa akizungumzia juu ya hoja ya uhalali wa Rais wa Mungano wa Tanzania, ambaye ndie aliyempa haki na yeye akiwa ni mshiriki katika uchaguzi uliomsababishia kuwa kiongozi kisha awe anathubutu kumuita mfalme.
Nae Yahya Kassim Issa, Mbunge wa Jimbo la Chwaka, alisema katika nchi zenye demokrasia ni Tanzania kwa kuwa na sifa ya kuwapa uhuru wa kutosha wananchi ambao wamekuwa wakipenda kuona kuwa wanabakia kuwa na amani.
Kutokana na hali hiyo Mbunge huyo alisema, tamko la Lissu linaleta mfarakano kwani Zanzibar ipo huru na ilipata serikali yake baada ya Mapinduzi, CHADEMA imeenda kwa ukoo katika viti vya wanawake ikiwa nchi itapewa uhuru watapoteza nchi.
Mbunge huyo alisema kutokana na hali hiyo ipo haja msajili wa vyama kukiangalia Chama hicho na ikiwezekana sasa kiwe mwisho Chumbe kwani Zanzibar CHADEMA hata matawi yake hayajulikani.
No comments:
Post a Comment