Habari za Punde

TUNATAFUTA MELI ZENYE UNAFUU KWA WANANCHI - MAALIM SEIF


Na Khamis Haji, OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema juhudi kubwa zinaendelea kuchukuliwa na serikali kuhakikisha zinapatikana meli za kisasa zenye uwezo wa kuchukua abiria wengi na zenye unafuu wa bei, kwa nia ya kuwarahisishia usafiri wa baharini
wananchi wa Zanzibar.

Maalim Seif alisema hayo jana alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari huko jijini Dar es Salaam, akiwa kwenye boti ya Kilimanjaro III aliyosafiria hadi Zanzibar.


Alisema hatua hizo zinachukuliwa kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Vitega uchumi Zanzibar (ZIPA), pamoja na juhudi kubwa za viongozi wa kitaifa, kwa nia ya kuondoa tatizo la uhaba wa meli na boti za abiria kati ya Unguja na Pemba, Tanga na bandari nyengine za Tanzania Bara.

Aidha, Makamu wa Kwanza wa Rais alisifu juhudi zinazochukuliwa na baadhi ya wawekezaji wazalendo katika kupunguza tatizo hilo, ikiwemo hatua ya kampuni ya Coastal Fast Ferries Ltd, ambayo hivi karibuni imeleta boti mpya ya Kilimanjaro III.

Alieleza kwamba hatua hiyo ni muhimu na kwa kiasi fulani imepunguza tatizo la uhaba wa usafiri na kuchangia kupatikana usafiri wa uhakika kwa abiria.

“Tunapongeza juhudi hizi, boti hii ya Kilimanjaro III imesaidia sana, lakini bado tunahitaji meli zenye uwezo wa kuchukua abiria wengi zaidi na mizigo, ambazo pia zitakuwa na unafuu wa bei, ambazo wananchi wetu walio wengi watazimudu”, alisema Maalim Seif.

Alieleza kuwa ni imani yake, juhudi hizo zinazoendelea kuchukuliwa zitaweza kuzaa mafanikio makubwa na baada ya muda si mrefu tatizo la usafiri wa baharini litapungua kwa kiasi kikubwa.
Maalim Seif alisema usafiri wa baharini kwa visiwa vya Zanzibar ni sekta muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii, hivyo serikali na sekta binafsi zitaendelea kutoa umuhimu wa kipekee katika kuiimarisha sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.