Habari za Punde

SIKU MOJA ZAIDI YAONGEZWA ZOEZI LA CHANJO KITAIFA

Na Juma Masoud

SERIKALI imesema imelazimika kuongeza siku moja zaidi, zoezi la chanjo kitaifa ili kukabiliana na matatizo yaliojitokeza katka zoezi hilo ikiwemo mvua za mfululizo.

Hatua hiyo ya serikali imetangazwa jana na Mkuu wa kitengo cha chanjo, Yussuf Haji Makame,ofisini kwake Wizara ya afya, kutokana na kubainika kwamba kuna watoto wengi zaidi walihitajika kupatiwa chanjo hiyo na wasingelimalizika katika muda wa siku tatu wa zoezi uliokuwa umepangwa awali.


Wastani wa watoto 898,745 walitarajiwa kupatiwa chanjo mwaka huu. Chanjo inayotolewa katika zoezi hilo ni pamoja na Surua, Polio, matone ya vitamin A na pia watoto wanaoshirikishwa katika zoezi hilo hupimwa hali ya ukuaji wao na wale wanaobanika kuwa makuzi yao hayende vizuri
wameandaliwa mpango wa kupatiwa uangalizi maalum ili kuhakikisha wanakuwa vizuri.

Zoezi la Chanjo lilianza jumamosi iliopita na kutarajiwa kufanyika kwa siku tatu za Jumamosi, Jumapili na jana jumatatu.

Uamuzi wa kuongezwa siku moja ya Chanjo kitaifa sasa zoezi hilo litaendelea tena leo kuhakikisha kwamba lengo lililopangwa la kuwapatia chanjo watoto wenye umri wa siku moja hadi miaka mitano linafikiwa kwa zaidi ya asilimia 95.

Uzinduzi wa chanjo kitaifa ulifanyika kijiji cha Muambe, Mkoani Pemba na Waziri wa Afya Juma Duni Haji kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed SAhein .

Mvua za vuli zinazoendelea kunyesha hasa sehemu za vjijini zimepunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya wazazi na wazee kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya chanjo katika maeneo mbalimbali.

Masheha katika baadhi ya maeneo walisema bado kulikuwa na idadi ndogo ya watoto ambao wangeweza kukosa kupatiwa huduma ya chanjo kutokana na matatizo ya mvua zinazoendelea kunyesha.

Hata hivyo, ofisa huyo wa Chanjo hakuweza kueleza mara moja ni wastani watoto wangapi ambao bado wamesalia bila kupatiwa huduma hiyo na wangapi walikuwa tayari wamepatiwa chanjo hadi zoezi hilo lilipofikia siku ya tatu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.