Malipo yote ya vilabu sasa kupitia benki
Na Salum Vuai, Maelezo
KUFUATIA misuguano ya mara kwa mara kati yake, vilabu na wadau mbalimbali wa mpira wa miguu nchini juu ya utendaji usioridhisha, Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa, kimeamua kujivua gamba taratibu.
Katika kuonesha kuwa sasa kinajenga uhalali wa kukubalika kwa wadau, chama hicho kimeamua kubadilisha mfumo wa kupokea malipo mbalimbali yanayolipwa na vilabu katika ofisi yake, na sasa malipo hayo yanatakiwa kupitishwa benki.
Kwa mujibu wa barua ya chama hicho ya jana Novemba 8, 2011 iliyotumwa kwa makatibu wa vilabu vya ligi kuu (premiar), daraja la kwanza, la pili taifa na ofisi zote za ZFA wilaya za Unguja na Pemba, utaratibu huo utaanza kutumika kuanzia tarehe ya barua hiyo.
"Malipo yote ya ZFA Taifa yanatakiwa yalipwe kupitia benki na kwamba haitapokea fedha taslim kutoka mkononi mwa mtaka huduma", ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho Mzee Zam Ali.
Taarifa hiyo imefahamisha kuwa, baada ya muhusika kufanya malipo ya ZFA kupitia benki, atatakiwa kuwasilisha waraka unaoonesha amelipa (Pay slip) katika ofisi za ZFA Taifa.
Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo gazeti hili linayo nakala yake, malipo hayo yanapaswa kufanywa katika Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kupitia nambari za akaunti 021108000540 kwa Unguja na kwa upande wa Pemba ni 041103000153.
Chama hicho kimeziambia klabu hizo kuwa,utaratibu huo ni mzuri na wa kisasa, hasa katika suala zima la udhibiti wa mapato, na kwamba kutokana na mazoea, inawezekana mwanzo zitapata usumbufu lakini baada ya muda zitauzoea na kuufurahia.
Nakala za barua hiyo yenye nambari ya kumbukumbu ZFA/NV/VOL. V/211, zimepelekwa pia kwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) pamoja na Msaidizi Katibu Mkuu wa ZFA Taifa, Pemba.
No comments:
Post a Comment