Habari za Punde

LIGI KUU, DARAJA LA KWANZA ZASIMAMISHWA

Na Salum Vuai, Maelezo

MATUMAINI ya mashabiki wa soka Zanzibar kuanza tena kushuhudia uhondo wa ligi kuu na ile ya daraja la kwanza taifa wiki hii, yamefutika.

Hali hiyo inafuatia hatua ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa, kutangaza kuzisimamisha ligi hizo kwa muda usiojulikana.

Taarifa ya kusimamishwa kwa ligi hizo imo ndani ya barua fupi ya Novemba 7, 2011 iliyotumwa kwa makatibu wa vilabu husika.


"ZFA Taifa imeamua kuzisimamisha mechi zenu zote mpaka hapo baadae", ilisema barua hiyo na kuhitimisha kwa kuomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.

Baada ya kuiona barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa ZFA Taifa Mzee Zam Ali, Zanzibar Leo liliwasiliana naye kutaka ufafanuzi juu ya sababu za hatua hiyo, lakini akasema kumejitokeza matatizo kidogo ya kiufundi yanayohitaji kusawazishwa.

"Ni kweli tumeamua kusimamisha ligi hizo kutokana na sababu kadhaa za kiufundi ambazo tunazifanyia kazi, na ishaallah haitachukua muda mrefu mashabiki wataanza tena kupata burudani viwanjani", alisema Zam kumwambia mwandishi wetu kwa njia ya simu.

Hata hivyo, hakuweza kuzitaja kasoro hizo, ingawa hakuwa tayari kuhusisha uamuzi huo na kadhia iliyotawala anga la soka katika siku za hivi karibuni, juu ya utata uliosababishwa na klabu ya Malindi kugomea ligi daraja la kwanza taifa na hatimaye kuuziwa daraja la ligi kuu, ingawa yenyewe inasisitiza haikununua bali hiyo ni haki yake.

Kwa muda sasa, hali ya hewa ya mchezo wa mpira wa miguu Zanzibar imekumbwa na shetani mbaya, ambapo siku moja baada ya kuzinduliwa ligi kuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad katika uwanja wa Gombani Pemba, mahakama ya mkoa Vuga iliamuru ligi hiyo isitishwe hadi hapo pingamizi la Malindi litakapopatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.