Habari za Punde

AJALI ZAUA 342, ZAJERUHI 3303 ZANZIBAR

Na Hafsa Golo

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed amesema inakadiriwa kwamba kiasi cha vifo vya watu milioni 1.3 na majeruhi milioni 50 hutokezea kila mwaka ulimwenguni kufuatia
ajali za barabarani.

Alisema hayo alipokuwa akifungua warsha ya watumiaji wa barabara kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais iliofanyika katika ukumbi wa salama Bwawani.

Alisema vifo vinavyosababishwa na ajali barabarani vinatarajiwa kuongezeka kufikia milioni 1.9 ifikapo mwaka 2020.


Alisema kuwa ulimwengu unaweza kuzuia vifo milioni 5 na majeruhi milioni 50 kwa kuwekeza usalama barabarani kitaifa kikanda na kimataifa.

Mohammed alisema kuwa ajali za barabarani zinachangia kupunguza hali ya uchumi wa dunia (GDP) kwa asilimia 3 hadi 6 kwa mwaka.

''Licha ya kupoteza maisha lakini pia ajali za barabarani zinapunguza rasilimali za uchumi katika nchi,''alisema.

Hata hivyo, alifahamisha kuwa takwimu za ajali barabarani kutoka Makao Makuu ya jeshi la polisi Zanzibar zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2008 mpaka Machi 2011 jumla ya ajali 2568 zilitokea na
kusababisha vifo 341 na majeruhi 3303.

Aidha, alisema kuwa takwimu hizo ni za kushitua kwani zinazidi kuongezeka na kufikia kiwango cha juu ikilinganishwa na takwimu za ajali kuanzia mwaka 2005 hadi 2007 ambapo jumla ya ajali 2259
zilitokea ikiwa ni tofauti ya ongezeko la ajali 309 ukilinganisha na ajali zilizotokea 2008 hadi Mach 2011.

Pia alisema jumla ya majeruhi 2955 walipatikana kwa kipindi cha 2005 hadi 2007 kukiwa na ongezeko la majeruhi 3303 waliopatikana kutokana na ajali kuanzia mwaka 2008 hadi march 2011.

Mohammed alieleza kuwa takwimu hizo si jambo la kujivunia hata kidogo kwani taifa limepoteza maisha ya watu wengi na wengine kupata ulemavu wa kudumu na kuharibu harakati zao za maisha walizokuwa wakiziendeleza katika kutafuta maendeleo jambo ambalo limepelekea watoto na familia zao kujiingiza katika majanga na kuhatarisha maisha yao,kutokana na kukosa kipato cha kujikimu kimaisha.

Amezitaka taasisi zilizopewa mamlaka ya kusimamia usalama barabarani kuzingatia ushirikiano na jamii katika masuala ya usalama barabarani na kujenga uwelewa kwa wananchi na kuwajuilisha kuwa jukumu la
kusimamia usalama barabarani ni la kila mmoja.

Alisema changamoto zinazo ikabili serikali ni kutowa elimu kwa jamii ili iondokane na dhana potofu kuwa suala la kuepusha ajali barabarani si za kikosi cha usalama barabarani na wizara ya miundo mbinu pekeyao.

Kwa upande wa Waziri wa Miundombinu, Hamad Masoud alisema serikali inahakikisha kuimarisha miundombinu ya ujenzi wa barabara zinazojengwa kuwa zinakidhi viwango ikiwa ni pamoja na uimara, upana pamoja na kuweka alama za barabarani.

Alisema serikali inakazi kubwa kuhakikisha madereva wanafuata sheria zote zilizowekwa za barabarani ili kuepusha ajali za mara kwa mara.

Hamad alisema kuwa sasa imefika wakati wa kutovumiliana na vitendo vya ukiukwaji wa sheria za barabarani na sasa sheria itafuata mkondo wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.