Habari za Punde

FUTURE CENTURY MIKONONI MWA KAMATI TENDAJI ZFA

Wakutana Jumamosi kuanika michango, matumizi fedha za Zanzibar Heroes

Na Salum Vuai, Maelezo

KIKAO maalumu kinatarajiwa kufanyika Disemba 24, kati ya Kamati Tendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na kampuni ya Future Century Limited ili kupata taarifa za fedha zilizochangishwa kwa ajili ya kuiendeleza timu ya taifa ya soka Zanzibar Heroes.

Kuitishwa kwa kikao hicho kunafuatia agizo la serikali kupitia Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), baada ya kuwepo malalamiko kwamba Zanzibar Heroes ilishiriki michuano ya Chalenji katika mazingira magumu licha ya fedha nyingi kukusanywa kwa ajili yake.


Kwa mujibu wa Msemaji wa ZFA Taifa Hafidh Ali Tahir, kikao hicho kitakachowahusisha wajumbe wote wa kamati tendaji Unguja na Pemba, kimepangwa kufanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani wakati wa asubuhi.

Hata hivyo, amesema muda wa kikao hicho unaweza kusogezwa mbele, kutegemea ni wakati gani wajumbe wa kamati hiyo kutoka Pemba wanaotarajiwa kuwasili siku hiyo hiyo, watafika kisiwani hapa.

Tahir amefahamisha kuwa, ajenda kuu za kikao hicho, ni kupata ufafanuzi wa mkataba unaohusu fedha zinazotafutwa kwa ajili ya kuiendeleza timu hiyo ya taifa, pamoja na uwazi juu ya fedha
zilizokusanywa wakati wa hafla ya chakula cha usiku Machi 26, mwaka huu katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort.

Alifahamisha kuwa mbali na kutaka kujua ni kampuni, taasisi na watu gani waliochangia au kuahidi kutoa fedha kwa ajili ya Zanzibar Heroes, Kamati tendaji ya ZFA pia itataka kufahamu kwa kina kiasi ilichopatikana na namna fedha hizo zilivyotumika.

“Tumeamua kuwaita viongozi wa Future Century ili tukae pamoja na kamati yetu tendaji, kwa lengo la kufahamishwa na kuhusu michango ya Zanzibar Heroes, na kujua vipi fedha zinazopatikana zinainufaisha timu yetu”, alifafanua Tahir.

Kampuni ya Future Century iliingia mkataba na ZFA kwamba itafanya kazi ya uwakala wa kuitafutia wadhamini timu ya taifa Zanzibar Heroes,ambapo pia ilimleta kocha Stewart John Hall kutoka Uingereza kukinoa kikosi hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.