MKUU wa kitengo cha hifadhi ya mtoto Zanzibar, Maria Obel Malila, amesema jukumu la kumlinda na kumuhifadhi mtoto ni la kila taasisi na sio la taasisi moja peke yake kama ilivyozoeleka katika jamii.
Alisema ushirikiano wa taasisi hizo unaweza kuibua na kujua taarifa mbali mbali ambao zilizokuwa zimefichwa katika taasisi moja au ndani ya jamii kutokana na imani iliyomondani ya jimii hiyo.
Maria Obel, aliyaeleza hayo, katika ukimbi wa kiwanja cha michezo Gombani wakati alipokuwa akiwasilisha mada, juu ya uratibu, wajibu na majukumu ya vyombo vinavyoshughulikia watoto, katika mafunzo ya siku nne, kwa wajumbe wa kamati ya hifadhi ya mtoto Pemba.
Alisema pindi taasisi hizo zitakapofanya kazi pamoja kwa mashirikiano, kadhia ya kudhalilishwa watoto nchini inaweza kuondoka.
Alieleza kuwa, kila taasisi, iliyoko katika jamii ina wajibu wa kumlinda na kumuhifadhi mtoto, kwani mtoto anapaswa kulindwa na kila taasisi iliyoko katika jamii.
“Suala la kumlinda mtoto ni suala kubwa linalohitaji mashirikiano ya kila aina, hivyo kila taasisi kwa mujibu wa fani zao inaweza ikamlinda,” alisema Maria Obel.
Aidha alisema mivutano na migongano katika utendaji wa kazi sio jambo zuri kuwepo katika kupigania kadhia hiyo, kwani ili kuweza kufanikisha suala la kumlinda na kumuhifadhi mtoto ni vizuri kuondosha mivutano na
migongano katika sehemu za kazi.
Alisema pale itakapotokezea mivutano basi masuala ya kumlinda na kumuhifadhi mtoto yapewe kipaombele kwa sababu ndio lengo la kuepo kwa kamati ya hifadhi ya mtoto Zanzibar.
Akizungumzia mahakama na ofisi ya DPP,alisema taasisi hizo zina wajibu mkubwa na kuzitaka kuhakikisha kesi za udhalilishaji watoto zinapatiwa ufumbuzi wa haraka , sambamba upelelezi kwani kuzichelewesha kesi hizo zinapofikishwa katika taasisi zao waathirika wanakosa hata imani na taasisi hizo.
Kwa upande wa habari, alisema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kutoa taarifa hususan zile ambazo zimefichwa katika jamii, ili jamii kuweza kufahamu kadhia hiyo.
Mapema akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar, Halima Maulid Salim, aliwataka wajumbe wa kamati ya hifadhi ya mtoto Pemba, kujitolea kwa hali na mali katika utendaji wao wa kazi ili kuweza kuleta mabadiliko juu ya kupunguza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa watoto Pemba.
No comments:
Post a Comment