Habari za Punde

MAFUNZO, ZENJI FM ZATHIBITISHA KUSHIRIKI KOMBE LA NYERERE

Na Mwajuma Juma

TIMU za mpira wa wavu za Mafunzo na Zenji FM zimethibitisha kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya Kombe la Nyerere.

Mashindano hayo ambayo yamepangwa kufanyika mkoani Moshi kuanzia Disemba 14 mwaka huu, yameandaliwa na Chama Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA).


Kwa mujibu wa Katibu wa Wavu wilaya ya Mjini, Ameir Msimu, tayari wameshapokea barua za uthibitisho wa mashindano hayo kwa timu mbili hizo ambazo zitaondoka kati ya tarehe 7 au 8 kuelekea mkoani humo.
Alisema kuwa awali mashindano hayo yalikuwa yafanyike Disemba 2 mwaka huu, lakini yaliahirishwa hadi Disemba 14 mwaka huu.

“Tayari timu zote zimeshathibitisha ushiriki wao katika mashindano hayo, na kinachosubiriwa ni siku ya safari pekee”, alisema.

Alisema kuwa tayari timu hizo zimeshaanza kufanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo ambapo anamatumaini makubwa ya kuweza kutwaa ubingwa huo.

“Pamoja na kuwa ni Katibu wa Chama hichi, lakini nikizungumza kama kocha wa Mafunzo pamoja na Mlezi wa Zenji FM nasema timu zote zipo makini na nina matumaini makubwa ya kufanya vyema”, alisema.

Alisema kuwa kwa upande wa timu ya Mafunzo wanatarajia kuondoka na wachezaji 10 na Zenji Fm wachezaji saba pamoja na viongozi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.